Akes Don afunguka kuhusu alivyofananishwa na mbwa na Sat B

Akes Don na Sat B ni wasanii wa nyimbo za miondoko ya Afrobeat kutoka nchini Burundi.

900
Akes Don, msanii wa Burundi

Msanii kutoka Burundi Akiman Espoir almaarufu Akes Don amewataka wasanii wawe na subira hasa wanapochanwa mitandaoni na mashabiki wa mahasimu wao kwenye muziki.

Katika mahojiano na Habari Pevu, Akes amesema “mimi nachanwa kila siku hasahasa na mashabiki wa Sat B ambao hawataki kuona napata maendeleo, nikipost kitu lazima natukanwa”

Msanii wa ‘kizunguzungu’ amesema angekuwa na moyo mwepesi angekuwa ameshatoweka kwenye sanaa za muziki, akisema hiyo imeanza mwishoni mwaka 2015 alivyofananishwa na mbwa mtandaoni na msanii mwenzake, Sat B.

“Wakati Sat B alipokuwa hapa Rwanda, Burundi palikuwa hakuna staa mimi nikawa nafanya kazi kwa bidii hadi kutoa video mbili kwa mwezi, ikaja kuonekana mimi ndio msanii ambaye nimebaki uwanjani, yeye hayupo, akina Fizzo walikuwa hawapo.”

“Sat B alichukua ka-mbwa ambako kamevaa miwani akawa ameandika jina langu mimi, akaposti Facebook, lakini baadaye akaifuta ile post, ila akawa amechukua screenshot, japokuwa kaifuta hiyo post lakini screenshot imezagaa sana katika makundi ya Whatsapp.”

Mvutano baina ya mashabiki wa Akes Don na wale wa Sat B ulianzia hapo na kuja kukolezwa moto na watangazaji walioikuza habari hiyo na kuifanya kuwa habari ya mjini.

“Walimshabulia kichizi kwenye comments baada ya watangazaji wa habari za udaku udaku kuunganisha picha yangu na picha ya Sat B na kutulinganisha…”

Akes Don amesema asingekuwa na moyo wa subira angekuwa ameshaacha muziki baada ya kuchanwa mitandaoni na mashabiki wa Sat B

Akes Don amesema lengo la Sat B ilikuwa ni kutafuta kiki baada ya kuona Akes Don ndiye anatamalaki usukani wa muziki nchini Burundi.

“Wakati alipofanya hicho alikuwa ana muda mrefu hayuko kwenye nchi, na ukipita muda mrefu upo nje ya nchi yako kimuziki unapotea, ndipo akaamua kutafuta kiki kupitia mimi.”

“Ilifika kipindi Warundi wakawa wamemsahau mimi nikawa ndo msanii mkubwa kwa Burundi mpaka watangazaji wa Burundi wakawa ndio wananizungumzia tu, kuna siku nilimpeleka Lolilo Tanzania kwa ajili ya shoo, mara Akes amefanya hiki, mara Akes ametoa wimbo, mara Akes…, yaani Sat B aliporudi akakuta jina langu ni kubwa akataka kunishusha kwa kunifananisha na mbwa ambaye amevaa miwani. Kipindi hicho nilikuwa hit, wasanii wengine wote walikuwa wamelala, baadhi wapo Burundi wengine wakiwa nje ya nchi…”

Kwa mujibu wa maelezo ya Akes, haikuishia hapo: “Tazama kuna video yangu na yake zilipostiwa siku moja, zilifanyiwa launch siku moja na eneo moja yaani kama nikifanyia barabara ya kwanza yeye anafanyia barabara ya tano, ikaonekana kuna upinzani hapo, sasa wale mashabiki zake wakawa wanataka kunishambulia sana.”

Licha ya kuingia kwenye mgogoro huo, Akes Don amesema hana kinyongo na Sat B na hata baada ya kashfa hiyo kutokea alimtengenezea wimbo wa ‘Hakuna matata’ tena alioshirikiana na ndugu wawili wa Akes, Chris na Junior.

“Sina kinyongo naye na nimeshamtengenezea wimbo akiwa na madogo zangu, halafu ukiniuliza kuhusu wasanii wa Burundi ninaowakubali hata yeye nitamtaja, Sat B ni msanii mkubwa ila hata yeye anajua alitafuta kiki kwangu na kila mtu anajua hilo.”

Akes Don yupo nchini Rwanda ambapo anatengeneza ngoma kama produza kwenye studio ya T-Time Production iliyoko Kicukiro, Jijini Kigali.

Alizaliwa Bujumbura mwaka 1993 na kuingia kwenye muziki akiwa na umri wa miaka 8 tu.

Jitihada zetu za kumtafuta Sat B ili aongee kuhusu madai ya Akes Don hazijazaa matunda.

Weka maoni