Askari wawili mbaroni kwa mauaji ya muuza baa Rwanda

492
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda, Luteni Kanali René Ngendahimana

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda, Luteni Kanali René Ngendahimana ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya muuza baa Ivan Ntivuguruzwa aliyeuawa kwa mapigo ya risasi.

“Kwanza nawapa pole wafiwa, kuondokewa na mtu ni kitu ambacho huwezi kumtakia mtu, hatuna budi kutoa pole kwani raia aliuawa na askari ulinzi, tuko pamoja na familia ya wafiwa katika kipindi hiki kigumu,” Lt Col Ngendahimana amesema.

Mashuhuda wa tukio la mauaji wameripotiwa kusema kuwa marehemu aliuawa alipozua purukushani baada ya askari kushindwa kulipia bia alizoagiza na kuzua zogo.

Mashuhuda wengine wamenukuliwa wakisema marehemu alizozana na askari huyo alipomkuta akitongoza mkewe ambaye alikuwa anafanya kazi kwenye baa hiyo.

Imeripotiwa kuwa taharuki hiyo ilisababisha askari mwingine aliyekuwa kwenye doria kuingilia kati na kisha kumpiga risasi nyingi marehemu akimtetea askari mwenzake.

Msemaji wa Jeshi ameepuka kuelezea mazingira ya mauaji hayo yaliyofanyika huko Gikondo Jijini Kigali usiku wa kuamkia leo, akiahidi kutoa taarifa zaidi baada ya upelelezi kukamilika.

“Imetokea majira ya saa saba za usiku wakati askari wakiwa kwenye doria maeneo hayo ya Gikondo, mmoja wao amempiga risasi raia na kusababisha kifo chake, hatujajua vizuri chanzo cha mauaji hayo ila naweza kukuhakikishia kuwa upelelezi umeanza na askari hao wawili wametiwa nguvuni ili kupisha juhudi za upelelezi,” amesema Lt Col Ngendahimana.

Mnamo Agosti 2014, mwanajeshi aitwaye Munyembabazi Théogene aliwafyetulia risasi watu waliokuwa kwenye baa moja huko Gicumbi Kaskazini mwa Rwanda na kuwaua watano huku akiwajeruhi wengine saba, baada ya kunyimwa penzi na msichana waliyekutana baa.

Bw Munyembabazi alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya mauaji, ambapo mahakama iliamua fidia ilipwe na familia yake na siyo serikali kwani hakuna aliyemtuma kuua.

Weka maoni