Bac T na Adam Mchomvu waiunganisha Rwanda na Tanzania

454
Bac T na Adam Mchomvu wakiwa studio wiki hii kabla ya Adam kurudi Tanzania

Mapema wiki hii marapa wawili ambao ni watangazaji pia, mmoja wa Rwanda mwingine wa Tanzania, Bac T na Adam Mchomvu, walirekodi wimbo walioshirikiana uitwao Tunaleta Vibe.

Wikiendi iliyopita Adam Mchomvu alikuwa Rwanda kwa ajili ya Rwanda Fiesta, kabla ya kurudi makwao ndipo yeye na Bac T wakarekodi wimbo huo wa kuhamasisha ushirikiano.

“Ni ngoma inayozungumzia East African connection sana sana ya Rwanda na Tanzania, halafu kwenye mistari tunabadilishana ujanja, nani anaweza zaidi,” amesema Bac T.

“Tumejaribu tu ku-flow, mimi najionyesha kama MC wa Rwanda, najisifia kivyangu, naye anajisifia kama msanii wa Tanzania,” ameongeza Bac T akizungumza na Habari Pevu.

Wasanii wa Rwanda wanaonekana kupenda kushirikiana na wale wa Uganda kuliko wa nchi zingine za Afrika Mashariki na hilo ni jambo lililo wazi hasa ukiangalia collabo wanazotoa.

Bac T aliyezaliwa ukimbizini nchini Tanzania na kukulia huko hadi aliporudi katika nchi ya asili ya wazazi wake mwaka 1999, anahamasisha ushirikiano imara kati ya Rwanda na Tanzania.

Endapo mambo yatanyooka, Bac T na Yvan Buravan wataiwakilisha Rwanda kwenye matamasha ya Serengeti Fiesta, kwani wote wamehakikishiwa hilo na Adam Mchomvu.

“Tume-set mambo yote, tumekuwa studio tumepata muda wa kuongea sana tumepanga projects za kutosha, ameniambia Fiesta mwaka huu na wewe lazima utakuwepo miongoni mwa watakaokuja,” amesema Bac T ambaye jina lake halisi ni Nkubiri Gerard.

Bac T anatambua kwamba Adam Mchomvu siyo muamuzi wa mwisho wa Fiesta, ila anaamini ahadi aliyompa itatimia kwani “Adam ni miongoni mwa wahusika wakuu wa maandalizi ya Fiesta.”

“Mara nyingi anakuwaga ni MC, anakuwaga ni rapa pia kwenye hizo Fiesta zao, ni mtu ambaye anakuwa kwenye kamati za wanaochukua uamuzi wa mwisho, kwa hiyo anaweza aka-suggest sidhani kama wengine wanaweza wakakataa, [na hiyo ya kumchukua Buravan] ameiongelea stage, mpaka aongelee stage na mabosi wake wote kama Ruge walikuwepo pale kwenye event, kwa hiyo hawezi kuongea vile na hana uhakika….”

Adam Mchomvu amvuta Buravan wa Rwanda 

Bac T ambaye alikuwa kidogo anaonekana ametoweka kwenye sanaa za muziki, ameiambia Habari Pevu kwamba kipindi cha ukimya wake alifanya kazi nyingi kinyemela ambazo atazitoa siku chache zijazo.

Yeye kufanya wimbo na Adam Mchomvu anaamini itamfikisha mbali kimuziki kwani Adam ni mtangazaji na msanii mkubwa kwa Tanzania, kwa mujibu wa maelezo yake.

Weka maoni