Mbunge Bamporiki atoa ya moyoni: tusipoidhibiti serikali historia itatuhukumu

366
Mbunge Edouard Bamporiki ambaye yupo bungeni kwa tiketi ya Chama Tawala cha RPF-Inkotanyi

Rwanda – Mbunge Edouard Bamporiki (RPF-Inkotanyi) amewataka wabunge wenzake waukumbuke wajibu wao wa kuidhibiti serikali, vinginevyo historia itawahukumu na kuwalaani.

Ametoa matamshi hayo baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/16 kutua bungeni.

Mdibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Obadiah Biraro, amesema ubadhirifu na ufujaji wa mali ya umma vimeigharimu serikali kitita cha faranga biliyoni 15.

Obadiah amesema kumekuwepo na mianya mingi ya upotevu wa mali ya umma na kusema inakera kuona watu wanarudia makosa yale yale waliyoyafanwa miaka iliyopita na kuonywa.

Mbunge Edouard Bamporiki amewakemea viongozi ambao hawajifunzi kutokana na ripoti za ukaguzi wa hesabu za serikali na badala yake huendekeza matumizi mabaya ya ofisi.

“Ningependa tubadili mienendo tuanze kuidhibiti serikali. Tusipoidhibiti awamu yetu itamalizika ila historia itabaki pale pale. Tunatakiwa tuidhibiti serikali turejeshe fedha zilizopotea, endapo hatutafanya hivyo historia itatuhukumu” Bamporiki amenukuliwa na Izuba Rirashe.

Ripori ya Obadiah Biraro imegusa hali ya hesabu za serikali katika taasisi 139, ambapo imeyamulika maeneo nyeti 14.

Taasisi hizo 14 ambazo zimeonekana kuwa na mianya ya upotevu wa fedha za umma ni pamoja zilitengewa asilimia 85% ya bajeti ya serikali na ni pamoja na RBC (ya afya), RAB (ya kilimo) REB (ya elimu), NAEB (ya mazao ya kilimo ya kuuzwa nje ya nchi), WDA (ya elimu ya ufundi)  RCS (ya magereza), RGB (ya uongozi bora), RTDA (ya ujenzi wa barabara), REG-EUCL na REG-EDCL (nishati), RURA (ya mawasiliano na usafirishaji), RDB (ya maendeleo), WASAC (ya maji) na RRA (ya mapato).

Mbunge Karemera Thierry amepigilia msumari kauli ya Bamporiki ambapo amedai kuchukizwa na utendaji kazi wa taasisi ambazo hazijirekebishi hata baada ya kuonywa.

Amewakemea viongozi wa taasisi hizo ambapo kila wakijitokeza bungeni kueleza ni kwa nini mali ya umma imefujwa au kubadhiriwa, huishia kuomba msamaha kila mwaka na kuahidi kwamba makosa hayatafanyika tena.

Weka maoni