Barafinda na Mwenedata waridhia uamuzi wa NEC

403
Fred Sekikubo Barafinda

Fred Barafinda, Gilbert Mwenedata wamesema hawawezi kubishana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwani wanatambua uhuru wa tume hiyo.

Wawili hao na mwanadada Diane Rwigara hawakuruhusiwa kugombea urais kama walivyotarajia.

NEC imesema hawajakidhi vigezo hasa kigezo cha sahihi za watu 600 kutoka wilaya zote 30, ambao wanathibitisha kumuunga mkono anayetaka kuwania urais.

NEC imesema ambao wamekidhi vigezo ni Paul Kagame (rais aliye madarakani), Frank habineza wa Chama pinzani cha Democratic Green Party na Philippe Mpayimana.

Uchaguzi wa rais nchini Rwanda unatarajiwa kufanyika tarehe 3-4 Agosti, 2017.

Bw Mwenedata na Barafinda wamesema ingawaje hawakupata kibali cha kugombea urais, lakini wataendelea kulitumikia taifa na kuishi vyema na Wanyarwanda.

Mwenedata amesema anaheshimu tume ya uchaguzi kwa hiyo yeye kama myarwanda ataendelea kufanya kazi zake kwa juhudi ili kuwatafutia wanyarwanda maendeleo thabiti.

Bwana Gilbert Mwenedata

Aidha Bw Mwenedata amedai kufurahishwa na kuona katika orodha ya walioidhinishwa na NEC kuna mgombea mwenzake huria ambaye ni Philippe Mpayimana.

Bw Barafinda akiongea kuhusu alivyoipokea taarifa isiyo nzuri ya yeye kutoidhinishwa kama mgombea, amesema kuwa Wanyarwanda wamekosa mwanasiasa mzuri.

Bw Barafinda amesema alifanya vyote ambavyo vilikuwa vikistahili kwa hiyo iwapo tume ya uchaguzi imeona kuna vigezo hajakidhi basi anakubaliana nayo.

2 Maoni

Weka maoni