Buffon, Messi na Cristiano Ronaldo kuwania tuzo ya mchezaji bora UEFA

289

Nyota watatu, Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na Gianluigi Buffon wameingia kwenye orodha fupi ya mwisho ya kuwania tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA).

UEFA imepunguza majina kutoka 10 hadi matatu leo, huku kinda wa Monaco, Kylian Mbappe na mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic wakiwa miongoni mwa waliokatwa.

Orodha hiyo fupi imeteuliwa na jopo la makocha 80 wa klabu zilizoshiriki hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa na Europa League msimu wa 2016-2017, pamoja na waandishi wa habari za michezo 55 walioteuliwa na kundi la waandishi wa habari za michezo Ulaya.

Ronaldo aliisaidia Real Madrid kutwaa taji la pili mfululizo la Ligi ya Mabingwa na kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo kwa mabao yake 12. Kipa Buffon aliiongoza Juventus kutwaa taji la sita mfululizo la Serie A, la tatu mfululizo la Kombe la Italia na kushika nafasi ya pili kwenye Ligi ya Mabingwa.

Anakuwa kipa wa pili tu kuingia tatu bora tangu kuanzishwa kwa tuzo hizo msimu wa 2010–2011, baada ya Manuel Neuer msimu wa 2013-2014. Messi alitwaa taji la Kombe la Mfalme maarufu kama Copa del Rey akiwa na Barcelona na akawa mfungaji bora wa La Liga kwa mabao yake 37 msimu uliopita.

Messi na Ronaldo wote wameshinda tuzo hiyo mara mbili, huku Mreno akiwa mshindi wa mwaka jana.

Weka maoni