Chama cha PL chafuata nyayo za PSD kumuunga mkono Kagame uchaguzi

340

Chama cha PL (Parti Liberal) nacho leo hii kimeamua kumuunga mkono Rais Kagame katika uchaguzi mkuu unaokaribia.

Kimefuata nyayo za chama cha PSD (Parti Socialiste Democrate) ambacho kilichukua uamuzi kama huo hapo jana Jumamosi.

PSD na PL ndivyo vyama ambavyo vina wanachama wengi nchini Rwanda baada ya chama tawala cha RPF-Inkotanyi.

Vyama hivyo vimesema Rais Kagame ndiye anafaa kuendelea kuiongoza Rwanda.

Wanachama wa vyama hivyo wametakiwa kumnadi na kumpa kura rais Kagame kwani vyama vyao vimejipanga nyuma ya rais huyo ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2000.

Hata hivyo, Chama cha RPF-Inkotanyi bado hakijamuidhinisha Rais Kagame kama mgombea wake.

Uchaguzi wa kumsaka atakayekiwakilisha chama cha RPF-Inkotanyi kwenye kinyang’anyiro cha urais umeanzia vijijini.

Pamoja na kwamba mgombea rasmi wa RPF-Inkotanyi hajajulikana, lakini inatarajiwa kuwa atakuwa Rais Kagame.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2015 katiba ya Rwanda ilirekebishwa ili kumwezesha Rais Kagame kuwania awamu ya tatu.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mwaka 2016, Rais Kagame alisema ameyathamini maombi ya raia waliotaka aendelee kuiongoza Rwanda.

Akiongea na Jeune Afrika siku chache zilizopita, Rais Kagame alisema ataachia madaraka mwaka 2024 ikimalizika awamu ya miaka saba anayotarajiwa kuongoza akishinda uchaguzi mwaka huu.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema ushindi wa Rais Kagame ni wa wazi.

Mwasisi wa chama cha Democratic Green Party of Rwanda (DGPR), Frank Habineza, amesema atagombea urais mwaka huu.

Wengine waliotangaza nia ya kuwania urais ni wagombea binafsi ambao ni pamoja na Philippe Mpayimana na Diane Rwigara ambao majina yao ni mapya kwenye ulingo wa siasa nchini Rwanda.

Bw Mpayimana aliwahi kuwa mwandishi wa habari wakati Diane Rwigara alijizolea umaarufu kupitia matamshi aliyoyatoa baada ya baba yake mzazi Asinapol Rwigara kufariki dunia katika ajali ya barabarani mnamo Februari 2015, ambapo alisema kifo cha baba yake ni mauaji yaliyoratibiwa na serikali, madai ambayo serikali iliyatupilia mbali.

Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Agosti 3-4, 2017.

Pichani: Bi Donatile Mukabalisa, Mwenyekiti wa chama cha PL na Mwenyekiti wa Bunge la Rwanda pia. Picha/Umuseke.

Wazo moja

Weka maoni