Chama cha PSD kumuunga mkono Kagame uchaguzi mkuu

603
Rais Kagame

Chama cha Demokrasia na ustawi wa jamii (PSD) kimesema hakina haja ya kumteua mwanachama wake kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaokaribia, na kuamua kumuunga mkono Rais Kagame.

Wanakamati wa kamati ya siasa ya chama hicho wamekutana leo hii maeneo ya Kacyiru Jijini Kigali kuzungumzia mustakbali wa chama hasa suala zima la mwakilishi wa chama kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti, 2017.

Waliohudhuria mkutano huo wametoa hoja ya pamoja kwamba mgombea wao ni Rais Kagame kutoka chama tawala cha RPF-Inkotanyi, wakisema ndiye anafaa kuendelea kuiongoza Rwanda.

Rais Kagame amekuwa madarakani tangu mwaka 2000.

Chama cha PSD ni cha pili kwa kuwa na wanachama wengi nchini Rwanda baada ya RPF-Inkotanyi.

Katika kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Dkt Vincent Biruta, leo hii, chama hicho kimesema Rais Kagame anaongoza vizuri na hivyo hawaoni sababu ya kumtafuta rais mwingine.

Mwenyekiti wa PSD, Dkt Vincent Biruta akieleza ni kwa nini chama chake kitaungana na chama tawala cha RPF-Inkotanyi kumnadi Rais Kagame

Chama hicho ni miongoni mwa vile vilivyoliomba bunge lirekebishe katiba ya Jamhuri ya Rwanda mwaka 2015 ili kumruhusu Rais Kagame kuwania awamu ya tatu.

Kwa mujibu wa katiba iliyorekebishwa mwaka 2015, Rais Kagame anaweza kuendelea kuiongoza Rwanda mpaka mwaka 2034.

Rais Kagame anasifika kwa kuiongoza vizuri Rwanda na kuiwezesha kupata maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali baada ya nchi hiyo kughubikwa na mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi yaliyofanyika mwaka 1994 na kugharimu maisha ya watu zaidi ya miliyoni moja na elfu sabini, kwa mujibu wa takwimu za Serikali ya Rwanda.

Weka maoni