Dau la usajili la Neymar kocha Arsene Wenger atia neno

222

Kocha wa Klabu ya Arsenal, Arsene Wenger ameonekana kukerwa na mwenendo wa vilabu barani Ulaya kwa kushindana kwenye usajili wa gharama kitu ambacho amedai kinakiuka sheria za FIFA na kupoteza ladha ya soka.

Mzee Wenger amesema yeye anaamini kuwa hakuna mchezaji mwenye thamani ya Euro milioni 100 duniani lakini kutokana na umiliki wa hisa za makampuni makubwa kwenye vilabu ndio chanzo cha vilabu vingi kutumia pesa nyingi kwenye usajili.

Kocha huyo ambaye amesaini miaka miwili kuendelea kuinoa Arsenal, amesema yeye hawezi kushindana na vilabu hivyo ikiwemo klabu ya PSG ambayo inaonekana kutumia pesa nyingi kununua wachezaji kwani timu hiyo na nyingine nyuma ya pazia kwenye wadhamini wao kuna mataifa yanafadhili ili yapate heshima duniani kwa kutajwa na sio kwa kupata faida hivyo ni ngumu kushindana nao kwenye usajili.

“Kwa upande wangu mimi ni ndoto kusajili mchezaji kwa bei ghali nitabaki kuwa msimamo wangu kama zamani hii ni kutokana na misingi ya klabu yangu na mambo haya yamekuja baada ya nchi kuanza kuwekeza kupitia vilabu, Hii inakuwa ngumu sana kuheshimu sheria za kifedha zilizowekwa na FIFA, Hebu fikiria kama nchi ina ubia na klabu ndogo halafu ikahitaji kumnunua mchezaji mkubwa ili ipate heshima itashindwa? hilo litawezekana hata iwe klabu ndogo na hii sio kwa ajili ya uwekezaji bali ni kwa sababu ya nchi fulani kutaka umaarufu tu”,amesema Arsene Wenger kwenye mahojiano yake na kituo cha runinga cha ESPN.

Hata hivyo, Wenger amesema yeye ataendelea kuheshimu sheria za FIFA kwani anafanya hivyo kwa kuwekeza na sio kwa kusaka heshima huku akiibeza PSG kwa usajili wa Neymar kwa kuita ni usajili usiokuwa na mtazamo wa kiuchumi kwani ni kitendo cha kuongeza mfumko wa bei za wachezaji zisizokuwa za msingi.

Kwenye dili la usajili wa Neymar wa Euro Milioni 222 inaaminika kuwa nyuma yake kuna mkono wa nchi ya Qatar yenye lengo la kurejesha imani kwa mataifa mengine baada ya kutengwa na baadhi ya mataifa kwa kudai nchi hiyo inafadhili magaidi.

Mtazame Wenger Hapa.

 

Weka maoni