Diamond Platnumz amvisha nyota Magufuli Rwanda

603
Diamond Platnumz akihojiana na waandishi wa habari mjini Kigali leo. Picha/Umuseke

Msanii wa Bongo Fleva ambaye yupo nchini Rwanda, Diamond Platnumz amesema hawezi kubishana na Magufuli kuhusu watoto wa kike wanaotungwa mimba kutorudi shule.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli, aliagiza kwamba wasichana wanaopachikwa mimba wakiwa masomoni wasiruhusiwe kuendelea na masomo.

Magufuli alisema “baada ya kufanya hesabu kidogo, atakuwa akimuomba ruhusa mwalimu kuenda kumnyonyesha mtoto anayelia.

Diamond amesema yeye kama msanii haoni sababu ya yeye kukosoa uamuzi uliochukuliwa na kiongozi ambaye alichaguliwa na wananchi baada ya kukubaliana na akili zake.

“He is the president, so siwezi kubisha, mpaka alipochaguliwa kuwa rais, ina maana tumekubaliana na akili yake tumeona anafaa,” amesema Diamond.

Aidha Diamond amesema “siwezi kujua ni kwa sababu gani mpaka (Magufuli) amesema hivyo” na kuongeza kuwa anaamini agizo la rais limelenga maslahi ya watanzania.

Mashirika ya kupigania haki za wanawake yamemtaka Rais Magufuli aombe msamaha kwa uamuzi wake huo.

Waziri wa mambao ya ndani Mwigulu Nchemba, ametishia kuyapokonya vibali vya usajili mashirika hayo.

Abdul Naseeb ‘Diamond Platnumz’ yupo Rwanda kuanzia jana, ambapo amekuja kwa ajili ya shoo ya Rwanda Fiesta ambalo litafanyika mjini Nyamata wilayani Bugesera, Julai 2.

Leo hii (Ijumaa) amekutana na waandishi wa habari kuzungumzia alivyojipanga, ndipo akaulizwa kuhusu agizo la rais, yeye kama msanii na mzazi wa mtoto wa kike pia.

Baada ya kusema kwamba maamuzi ya rais aliyechaguliwa na wananchi hayapingiki, Diamond ameongeza, “Another thing, wakati mwingine mtu kusema kitu, anapotoa kitu huwezi kujua amekutana na ushahidi gani. Nikupe mfano, mtu unaweza kumuuliza ‘nikukate kidole au kichwa?’, anasema ‘nikate kidole’, ukikata kidole mtu mwingine anasema we vipi mbona umekata kidole na siyo kichwa? No! Nakubaliana naye, na I am a musician, I am not a politician.”

Diamond akiwa na wasanii wa Rwanda atakaotumbuiza nao, ambao ni Dj Pius, Charly na Nina

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, msichana anayebeba mimba akiwa bado masomoni haruhusiwi kurudi shule, na mume aliyempa mimba hiyo huhukumiwa kifungo cha miaka 30.

Baada ya kuongea na waandishi wa habari, Diamond ameenda Goma ambapo anatarajiwa kufanya shoo kesho jumamosi, na kutoka Goma ndipo atarudi Kigali kwa ajili ya tamasha la Rwanda Fiesta litakalofanyika huko Bugesera, Golden Tulip Hotel, nje kidogo ya Kigali.

Weka maoni