Diamond Platnumz atua Kigali, aahidi burudani isiyo kifani

510
Diamond Platnumz akihojiana na watangazaji mjini Kigali

Nguli wa muziki wa Bongo Fleva Abdul Naseeb almaarufu Diamond Platnumz amewasili mjini Kigali jioni ya leo (Alhamisi) kwa ajili ya tamasha litakalofanyika mwishoni mwa wiki hii.

Waandishi wa habari na wapiga picha lukuki walikuwa wanamsubiri katika uwanja wa ndege wa Kigali ambapo walimuuliza maswali machache kwa muda wa dakika moja na nusu.

Hii ni mara ya pili Diamond Platnumz kufika Rwanda. Mara ya kwanza alifanya shoo ya kihistoria na kuwaacha hoi mashabiki wake katika egesho la magari la Petit Stade.

Kipindi hicho alikuwa na madansa 8 akiwemo Dogo Aslay wa kundi la Yamoto Band, ambao walimsaidia kutumbuiza nyimbo zake kwa muda wa masaa karibia mawili.

Diamond ameahidi burudani kali

“Raundi hii nimekuja na team kubwa, nina bendi, dancers, nyimbo tofauti, so (mashabiki) wasubiri vitu vizuri,” amesema Chibu Dangote katika mahojiano na watangazaji leo.

Diamond ameahidi kuwapagawisha wapenzi wa muziki wake na kuwataka waje na viatu vitakavyowawezesha kukatika na muziki na leso za kufuta machozi pia.

“Nafikiri waje na viatu vitakavyowawezesha kucheza kwa sababu tutakuwa tunaimba na kucheza pamoja kama unavyojua mimi nina nyimbo nyingi za kucheza,” amesema.

“Waje na leso pia kwa sababu tutakuwa na nyimbo zingine za huzuni kwa hiyo watalia,” ameongeza Diamond akimjibu mwandishi wa Habari Pevu.

Gari lililomsafirisha Diamond toka uwanja wa ndege kwenda hotelini

Tamasha la Kigali Fiesta ambalo amealikwa limeandaliwa na Cloud TV Rwanda. Litafanyika huko Nyamata wilayani Bugesera, Golden Tulip Hotel, nje kigodo ya mji wa Kigali.

Wasanii wengine wanaotarajiwa kuwepo ni pamoja na Vanessa Mdee, kundi la Morgan Heritage, kundi la Charly na Nina na msanii Dj Pius.

Weka maoni