Dkt Munyakazi aikosoa mahakama, agoma kuongea mpaka mwisho wa kesi

323
Dkt Munyakazi anaona haifai kuendeshea kesi yake katika chumba ambacho ndani yake hamna picha ya rais wa Rwanda (Picha/Umuseke)

Dkt Léopold Munyakazi anayetuhumiwa kwa kuhusika na mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Watutsi nchini Rwanda, amegoma kuzungumza mahakamani mpaka mwisho wa kesi akidai mahakama kufanya upendeleo.

Amemuambia hakimu wa Mahakama ya Muhanga anayeendesha kesi hiyo kwamba anaona kuongea kwake hakusaidii chochote kwani mahakama imeegemea upande wa waendesha mashtaka.

Dkt Munyakazi alirudishwa Rwanda Septemba 2016 kutoka Marekani ambako amekuwa akiishi kwa muda wa miaka 12 hadi hapo mahakama ya Marekani ilipoamuru arejeshwe Rwanda ili awajibishwe kwa mujibu wa sheria za nchi yake.

Ameonyeshwa video ya mahojiano aliyompa mwandishi wa habari kabla hajarudishwa Rwanda, akizungumzia maisha yake kabla ya mauaji ya kimbari na baada ya mauaji hayo.

Katika video hiyo iliyoletwa mahakamani na waendesha mashtaka, anasikika akielezea alivyoteswa mpaka kufukuzwa kazi na serikali kabla ya mwaka 1994, na alivyoteswa na serikali ya leo pia.

Baada ya kusikilizishwa mahojiano hayo, alisoma waraka wa kurasa mbili aliouandika kuhusu sababu za yeye kuamua kutoongea tena mahakamani, akiukosoa utaratibu mzima wa uendeshaji kesi.

Amesema kuna vitu vingi alitaka mahakama ivishughulikie, mahakama ikawa inatupilia mbali maombi yake, ikiwemo kuwaitisha marais wa nchi mbalimbali na viongozi wa UN ili na wenyewe wahojiwe.

Aidha mtuhumiwa huyu amesema aliitaka mahakama iendeshee kesi yake katika wilaya ya zamani ya Kayenzi (Kamonyi ya leo) ambako anadaiwa kutekelezea mauaji ya kimbari, mahakama ikakataa.

Mshukiwa huyu alisema hana imani na utendaji kazi wa hakimu ambaye hulipwa mshahara na serikali, akisema kwa vyovyote vile hakimu kama huyo ataegemea upande wa serikali.

Waendesha mashtaka wamesema Dkt Munyakazi kwa nyakati tofauti aliyakashifu mauaji ya kimbari yaliyofanyika dhidi ya jamii ya Watutsi akiyataja kuwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Makahama imesema aongee asiongee kesi itaendelea, kwa mujibu wa Umuseke

Kesi imeahirishwa hadi Julai 8, 2017.

Wazo moja

  1. Damu ni nzito kuliko maji, kama kweli aliua watu atagharamia, huwezi kuua mtu kama mbu, damu ya mtu siyo kama maji ya kumwagwa, ngoja tusiburi hukumu lakini

Weka maoni