Gatsibo: Walalamikia athari za kukosa migahawa

135
Ofisi ya Tarafa ya Nyagihanga wilayani Gatsibo

Wakazi wa tarafa ya Nyagihanga wilayani Gatsibo mashariki mwa Rwanda wanalalamikia ukosefu wa migahawa, ambapo hakuna mgahawa hata mmoja katika tarafa yao.

Ili kupata kinywaji au chakula, watu hulazimika kuenda tarafa jirani ya Ngarama ambapo nauli ni elfu tatu kwa usafiri wa pikipiki kwenda na kurudi.

“Hakuna soda wala ndizi mpaka niende Ngarama na ni mbali sana,” amesema Bwana Seromba Silver, ambapo ameitaka serikali ilitafutie ufumbuzi tatizo hilo.

Si raia wa kawaida tu ambao hutaabika kupata huduma za migahawani kwani hata wafanyakazi wa Tarafa ya Nyagihanga hulazimika kuenda huko Ngarama wanapotaka kupata chakula cha mchana.

“Hakuna mgahawa hapa, ambao wanaishi karibu na hapa hula nyumbani kwao, waishio mbali huenda huko Ngarama kwa kuwa hawana jinsi,” amesema mmoja wao.

Musonera Emmanuel ambaye ni Katibu Mtendaji wa Tarafa ya Nyagihanga amesema vilio vya raia vimekuwa vikisikika na hatua madhubuti za kuwatuliza wananchi zimeshachukuliwa.

Amesema wamekuwa wakiwatolea mwito wajasiriamali kuchangamkia fursa zilizopo na kujenga migahawa kwani wateja wapo kwa wingi.

“Ni kweli migahawa haipo ila kuna washiriki wetu ambao wana mpango wa kujenga, nataka niwaalike wiki hii tuzungumzie maendeleo ya tarafa yetu na nimewataka viongozi wa kata wanisaidie katika hilo,” amesema Musonera.

Bw Musonera anaamini atawahamasisha wawekezaji kuchangamkia ujenzi wa migahawa na baa na ana uhakika watamuelewa kwani wakazi wa Nyagihanga wana pesa.

Wafanyakazi wa tarafa husika wamewataka viongozi wao wawaruhusu wawe wanajipikia kwani kusafiri kwenda Ngarama kwa ajili ya chakula kunawaathiri kimwili na kisaikolojia.

Weka maoni