Gavana Mureshyankwano abubujikwa na machozi kusikia Watutsi walivyouawa

Simanzi na majonzi viliitawala nafsi ya Gavana Mureshyankwano kwa muda wa dakika moja ambapo alionekana akilia kwenye meza ya kutolea hotuba yake ya maombolezo.

527
Gavana wa Mkoa wa Kusini Rose Mureshyankwano akilia kwa uchungu kabla ya kutoa hotuba yake kwa waombolezaji

Gavana wa Mkoa wa Kusini nchini Rwanda, Rose Mureshyankwano, amepata wakati mgumu kusikia ushahidi wa kijana aliyenusurika kwenye mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.

Ushahidi wa Uwarurema Théoneste aliyepoteza ndugu watano na wazazi wake, ulimsikitisha Bi Mureshyankwano kiasi cha kumfanya alie huku amejiinamia.

Uwarurema ameeleza jinsi familia yao ilivyokimbilia katika Katoliki la Mugina wilayani Kamonyi kabla ya wao wote kuvamiwa na kuuwa kinyama.

Amesema yeye tu ndiye aliponea chupuchupu, ambapo ndugu zake watano walishuhudia tukio la mama yao kuuawa kwa kurushiwa guruneti kabla ya wao na baba yao pia kuuawa kesho yake.

Bw Uwarurema amesema mauaji hayo yaliyofanyika Aprili 26, 1994, yalitekelezwa na wanamgambo wa Interahamwe kwa ushirikiano mkubwa wa wakimbizi wa Kirundi.

Warundi hao walikuwa wamekimbilia Rwanda kufuatia machafuko ya kisiasa yaliyoghubika taifa lao hasa baada ya Rais wao Melchiol Ndadaye kuuawa na wanajeshi mnamo Oktoba 1993.

Siku za kuanza za mauaji ya kimbari, Watutsi waliotafuta hifadhi kwenye kanisa la Mugina walijibu mashambulizi ya Interahamwe wakiwa na ushirikiano wa mkuu wa wilaya.

Ilibidi vijana wa Interahamwe wamuue kwanza Mkuu wa Wilaya ya Mugina, Ndagijimana Callixte, ili kufanikisha uvamiaji wa Watutsi ambao alikuwa amesimama kidete kuwatetea.

Baada ya kumuua wakaitwa Warundi kutoka kambi ya Wakimbizi ya Nyagahama. Walikuja na kuanza kuauwa Watutsi wa wilaya hiyo na wilaya jirani waliokuwa wamekimbilia sehemu hiyo.

Simanzi na majonzi viliitawala nafsi yake kwa muda wa dakika moja ambapo alionekana akilia kwenye meza ya kutolea hotuba yake ya maombolezo.

Gavanba Mureshyankwano amejiinamia kwa muda wa dakika moja kabla ya kutoa hotuba yake

Ushahidi huo uliomliza Gavana Mureshyankwano, umefuatwa na nyimbo za msanii Bonhomme ambazo zimewagusa sana waombolezaji na kuwafanya baadhi yao washikwe na kiwewe.

Mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaligharimu maisha ya watu zaidi ya miliyoni moja katika kipindi cha miezi mitatu tu tangu Aprili hadi Julai 1994.

Weka maoni