Gavana Mureshyankwano awakanya waandishi wa habari

202
Gavana Mureshyankwano akiongea na waandishi wa habari leo

Gavana wa Jimbo la Kusini nchini Rwanda, Bi Marie Rose Mureshyankwano amewataka waandishi wa habari kuepuka kukuza habari.

Ameeleza alivyochukizwa na habari iliyoandikwa kuhusu yeye kulia hadharani mnamo Aprili 2017, akisema haina unyayo wala utosi.

Mureshyankwano amesema mwandishi wa habari alitakiwa aandike vitu vingi vya maana vilivyozungumzwa kwenye tukio hilo na siyo habari isiyokuwa na tija kwa jamii.

Bi Mureshyankwano anakiri kuwa alilia, lakini, kwa mujibu wa maelezo yake, mwandishi wa habari hakuwa na sababu yoyote ya kujikita kwenye machozi kwani hayana maslahi kwa umma.

Ametoa matamshi haya leo hii katika mkutano wa mashauriano uliojumuisha waandishi wa habari, jeshi la usalama na viongozi wa jimbo la kusini.

Amesema, “Nataka niwaambie kitu kilichonikera, tulikwenda Kamonyi kwenye kumbukumbu, nililia kwa hisia ila kilichonihuzunisha ni kwamba aliyeandika habari hiyo alipuuzia vitu vya maana vilivyozungumzwa na spika wa bunge ambaye ndiye aliyekuwa mgeni mkuu kwenye tukio, nilijiuliza alichodhamiria kuwaelimisha wasomaji wake. Nadhani alitakiwa aandike alichoongea spika wa bunge kwanza na siyo kuchemsha vichwa vya wasomaji kwa kuongea ambayo hayakunyooka tu.”

Ameongeza, “Kabla ya kuwa Gavana mimi ni mwanadamu, nina haki ya kufurahi wakati wa furaha na kusikitika pia wakati wa dhiki, ila ukiandika machozi yangu kwenye kichwa cha habari huwa unadhamiria kumfundisha nini atakayesoma habari hiyo?”

Wakati wa kumbukumbu za mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi wilayani Kamonyi, Bi Mureshyankwano alitokwa na machozi baada ya kusikia ushahidi wa manusura.

Ushahidi wa Uwarurema Théoneste aliyepoteza ndugu watano na wazazi wake, ulimsikitisha Bi Mureshyankwano kiasi cha kumfanya alie huku amejiinamia.

Uwarurema alieleza jinsi familia yao ilivyokimbilia katika Katoliki la Mugina wilayani Kamonyi kabla ya wao wote kuvamiwa na kuuwa kinyama.

Alisema yeye tu ndiye aliponea chupuchupu, ambapo ndugu zake watano walishuhudia tukio la mama yao kuuawa kwa kurushiwa guruneti kabla ya wao na baba yao pia kuuawa kesho yake.

Gavana Mureshyankwano abubujikwa na machozi kusikia Watutsi walivyouawa

Wazo moja

  1. Maoni yangu ni kwamba Mwandishi wa habari naye ana haki ya kuchagua cha kuandika siyo gavana kumpa msitari wa kuandika .

    Naona gavana hapa anataka kujifanya mkosowaji wa uandishi wa habari .

    Watu wa Afrika hawajui jinsi media inavofanya kazi ,kwani mbona wa akina Barack Obama wariomyeshwa wakiwa wametowa machozi Na hawakulalamika ?

    Nami siwezi kuandika mengi nikiwa nimeona Gavana akilia kabisa watu wawe wanajua kwamba muandishi wa habari si machine wwnayoitumia vile wanavotaka mpaka gavana atowe wazo la alichotakowa kuandika mwandishi wa habari !!

    Namushangaa sana gavana huo tena namuhurumia sana kwa mentality yake inayojaa uzushi na upuuzi mtupu

Weka maoni