Hata FDLR watuvamie tukiwa usingizini sisi ndio tunashinda vita – Jenerali Ibingira

286
Luteni Jenerali Fred Ibingira akitoa hotuba yake kwa waombolezaji

Mkuu wa Jeshi la Akiba ambalo ni sehemu ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda, Luteni Jenerali Fred Ibingira, amesema waasi wa FDLR wanaolenga kuipindua serikali hawawezi chochote.

Ameipuuzia kauli ya mkuu wa waasi hao, Jenerali Victor Byiringiro aliyeahidi kupinduliwa kwa Serikali ya Rwanda kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti, 2017.

Amesema waasi hao walio misituni Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hawawezi kushinda vita hata wakiivamia Rwanda wakati jeshi likiwa limelala usingizi.

Ametoa matamshi hayo wakati akihutubia umati wa watu kwenye tukio la kuwakumbuka waliokuwa wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo ambao waliuawa kipindi cha mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994.

Amesema waliotekeleza mauaji ya kimbari wamekuwa wakitaka kutoa ushauri kuhusu jinsi Rwanda inavyotakiwa iongozwe huku wakitishia kuipindua serikali iliyopo, na kuitaja hiyo kuwa ni ndoto isiyoweza kutimia hata iweje.

Amesema, “wapo ambao mchana kutwa tunawasikia wakisema eti ‘tutavamia’, tumemsikia Byiringiro akisema wataipindua serikali hii kabla ya uchaguzi kuanza! Hata tusinzie vipi FDLR hawatuwezi, wamekuwa huko waliko kwa miaka 23 sasa hawajatembea hata umbali wa santimeta 1 halafu leo wanadai eti wataivamia Rwanda? Longolongo tu.”

Waasi wa FDLR ambao serikali ya Rwanda inawachukulia kama kundi la kigaidi, wamekuwa wakiomba jamii ya kimataifa isaidie kuweka meza ya mazungumzo baina yao na serikali ya Rwanda.

“Maneno ya hao walio nje ya nchi kuhusu jinsi ya kustawisha taifa ni longolongo tu, mnawajua waliwahi kuwa wanasiasa nchini humu kwa nini hawakufanya wanavyotaka vifanyike leo? Eti ‘FDLR wanatakiwa warudi waiongoze nchi,’ viongozi wake wanajulikana, Mudacumura ndiye alitekeleza mauaji ya kimbari hapa, Iyamuremye mnamfahamu pia, si ndio hao?” ameongeza Luteni Jenerali Fred Ibingira.

Amesema waasi hao na watetezi wao hawatafikia malengo yao ya kuipindua serikali iliyopo madarakani, na amewapongeza baadhi yao ambao wamesalimu amri na kurudi nchini.

Luteni Jenerali Fred Ibingira amesema baada ya Rwanda kukombolewa mwaka 1994 kutoka mikononi mwa serikali iliyoratibu na kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi, yamefikiwa maendeleo katika sekta mbalimbali na usalama umehakikishwa hakuna awezaye kuuhatarisha.

Chanzo: Igihe

Weka maoni