Kaburi la Ivan Semwanga kufukuliwa? Mrundo wa pesa alizozikwa nazo zimezua utata

925
Zilimwagwa pombe na noti kwenye jeneza la Ivan Semwanga

Shirika la  haki za binaadam nchini Uganda limemuomba Wakili Mkuu wa serikali atoe maoni yake kuhusu mwili wa tajiri Ivan Semwanga kuzikwa na noti Jumanne wiki hii huko Kampala.

“Wanayaweka maisha ya familia ya Semwanga kwenye hali ya hatari, nani ataendelea kulilinda hili kaburi? Bila shaka watu watakuja walifukue hili kaburi,” amesema Gideon Tugume ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo la kupigania haki za binadamu nchini Uganda.

“Wakili Mkuu wa Serikali anatakiwa atupe maoni yake kuhusu jambo hili,” ameongeza Tugume, kwa mujibu wa New Vision.

Ivan Semwanga ambaye ni baba wa watoto watatu  wa kiume ,alikuwa mfanyabiashara mashuhuri nchini Uganda na nchini Afrika Kusini. Marehemu Semwanga alikuwa mume wa Zari Hassan na baadae kutengana kabla ya kifo chake. Zari Hassan  kwa sasa yupo kwenye mahusiano ya kimapenzi na nguli wa muziki wa Bongo Fleva Diamond Platnumz.

Siku ya mazishi yake watu walipigwa na butwaa na bumbuazi baada ya matajiri  wenzake kutoka kundi  la Rich Gang kujitokeza na kuanza kuzambaza mrundo wa noti ndani ya kaburi kabla ya kuingizwa jeneza.

Kitendo hicho kimezua gumzo mitandaoni kuhusu uhalali wa kuzikwa na pesa mwili huo wa marehemu, tukio ambalo limekemewa na  wengi  huku baadhi ya wenzake wakiunga mkono kwa kigezo cha kuonyesha ufahari aliokuwa nao marehemu wakati yuko hai.

Kutokana na baadhi ya vijana kuwa na mipango ya kufukua kaburi la Ivan ili waweze kutoa mamiliyoni ya pesa aliyozikwa nayo, maafisa usalama wameweka ulinzi maalum kwa ajili ya Kaburi hilo.

Polisi  wameonekana katika doria jirani  na kaburi hilo la Ivan, huku wengine wakiwa wameketi chini ya mti karibu na eneo hilo.

Ulinzi wa jeneza la Ivan umehakikishwa

Jimmy Luyinda ambaye ni mkuu wa familia ya Semwanga, amesema polisi hao wataendelea kulinda Kaburi hilo kuhakikisha halifukuliwi mpaka litakapojengewa uzio mkubwa.

Huku haya yakiarifiwa, baadhi ya wanafamilia ya marehemu wamesema hawaamini kwamba kweli amefariki dunia.

 

Baadhi ya waliojitokeza kushuhudia mazishi ya Ivan
Marehemu semwanga alizaliwa mwaka 1977

2 Maoni

  1. Hao matajiri hawana akili inakuwaje mpaka unamzika mtu na pesa? wapo watu wengi ambao chakula wanakitafuta jalalani unashindwa kuwahudumia watu kama hao unaiweka pesa kwenye jeneza ili iweje sasa? Mafala hao

  2. KWA MAANA PESA HIZO HUWA ZINATOKA GIZANI WAMEAMUA ZIRUDISHWE ZILIKO TOKA HUWA HAZIPATIKANI KWA NJIA HALALI!

Weka maoni