Kagame kuongea mubashara na wananchi redioni kuelekea uchaguzi wa urais

323
Rais Kagame akiongea na waandishi wa habari Alhamisi wiki hii baada ya kuwasilisha nyaraka za kuomba kuruhusiwa kuwania urais (Picha/Village Urugwiro)

Rais wa Rwanda Paul Kagame atakuwepo mubashara kwenye kipindi kitakachoruka katika runinga na redio vya taifa hapo kesho jumapili, saa tisa za alasiri saa za Rwanda (saa saba GMT).

Anatarajiwa kuzungumzia masuala mbalimbali yahusuyo mustakbali wa taifa hilo la Afrika ya Kati, na raia wataruhusiwa kuuliza masuali ambapo atayajibu papo hapo.

Mkurugenzi wa Shirika la Habari la Taifa (RBA), Arthur Asiimwe, amewataka wananchi waanze kutuma maswali yao kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kutumia hashtag ya #RBAHostsKagame

Baada ya Bw Arthur kutoa taarifa hiyo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, imesambaa katika makundi ya Whatsapp na Facebook na kuwa gumzo nchini kote.

Amewajulisha waishio nje ya Rwanda kuwa wanaweza kutizama runinga ya taifa (RTV) kuwa kipindi kitapeperuka mubashara katika tovuti ya TVR ambayo ni http://rba.co.rw/tv

Alipoulizwa kama kuna mada maalum ambayo itazingatiwa katika kuuliza maswali, Bw Assimwe amesema rais amejipanga kuyajibu maswali yoyote yale na kuwataka watu waepuke maswali ya upuuzi.

Hii itakuwa ni rekodi ya kihistoria kwa RBA kwani hii itakuwa mara ya kwanza Rais Kagame kufika katika viwanja vya shirika la habari la Rwanda.

Contact FM ndiyo redio pekee ambayo Rais Kagame alialikwa na kuhojiwa, kwenye kipindi chake cha Cross Fire ambacho kilikuwa kinavuma kwa kishindo miaka karibia kumi iliyopita.

Ukiacha Contact FM, hakuna chombo kingine cha habari nchini Rwanda ambacho Rais Kagame amekitembelea.

Haijajulikana kama kuna maswali ataulizwa na Cleophas Barore ambaye ndiye ataongoza kipindi hicho, au atayajibu tu maswali yatakayowasilishwa na raia kwa kupiga simu.

Cléophas Barore ambaye amelitangazia shirika la habari la taifa kwa zaidi ya miaka 20 ndiye atakayempokea studioni Rais Kagame.

Ikumbukwe kuwa hiki ni kipindi cha maandalizi ya kinyang’anyiro cha urais ambacho Rais Kagame anatarajiwa kutumia kuzinadi sera zake ili kuweza kupata kura za wananchi.

Uchaguzi wa urais utafanyika Agosti 3-4 2017.

Weka maoni