Kagame na Habineza ndio wameidhinishwa kugombea urais Rwanda

509
Rais wa Tume ya taifa ya Uchaguzi Rwanda, Profesa Kalisa Mbanda. Picha/Umuseke

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Rwanda leo hii imetoa taarifa kuhusu waliokubaliwa kugombea urais mwaka huu, ambapo Rais Kagame na Frank Habineza wa chama cha Green Party ndio wameidhinishwa.

Ambao hawajaidhinishwa ni wale ambao hawakukidhi vigezo, hasa kigezo cha kupata sahihi za watu wanaokuunga mkono angalau watu 12 katika kila wilaya.

Rais wa Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC), Profesa Kalisa Mbanda, amesema ambao hawajajaza sahihi zinazotakiwa wana hadi Julai 6 kuzikusanya na kuziwasilisha kwa NEC ili zichunguzwe.

Mnamo Julai 7 ndipo NEC itatoa orodha ya mwisho na isiyobadilika ya wagombea urais, karibia mwezi mmoja kabla ya uchhaguzi wenyewe kufanyika.

Fred Barafinda hajakabidhi kwa NEC orodha ya watu waliosaini karatasi zake kuthibitisha kuwa wanamuunga mkono, kwa mujibu wa maelezo ya NEC.

Mwanadada Diane Rwigara ambaye picha zake za utupu zilivuja mitandaoni mara baada ya kutangaza nia yake ya kugombea urais, alipata sahihi zaidi ya zile zinazotakiwa ila baadhi zimepuuziwa.

Profesa Mbanda amesema ingawaje alipata sahihi lukuki lakini kuna wilaya ambazo hakupata sahihi 12 na zingine ambazo alipata sahihi zaidi ya 12 ilhali sahihi za ziada hazihesabiwi.

Kuhusu Mpayimana, alipata sahihi 265 ambazo hazitoshi, huku kukiwa na wilaya 23 ambazo hakupata sahihi zozote.

NEC imesema Gilbert Mwenedata ambaye alianguka ubunge mwaka 2013, alipata sahihi 387 kutoka wilaya 15 tu.

Rwanda ina jumla ya wilaya 30 ambazo mgombea anatakiwa apate walau sahihi za watu angalau 12 wanaothibitisha kumpa uungaji mkono wao.

NEC imesema kuna sahihi ambazo haikuzithamini, ikiwemo zile ambazo kuna ukinzani kati ya wilaya ambayo mtu amejiandikisha kupiga kura na ile ambayo inaonekana kwenye kikaratasi cha mgombea.

Wengine eti waliandika vibaya namba za vitambulisho vyao vya uraia huku wengine walisaini kwa niaba ya wenzao. Sahihi kama hizo pia hazikuthaminiwa.

Wote ambao hawajakidhi kigezo cha sahihi ni wale wanaotaka kuwania urais kama wagombea binafsi.

Pamoja na kwamba NEC imesema ambao hawajapata sahihi za kutosha wana muda wa kuendelea kuzisaka, lakini inaweza isiwe rahisi kwao hasa ikizingatiwa mazingira waliyoyataja kuwa ni magumu.

Philippe Mpayimana alidai kuombwa hela na watu anaotaka wampe sahihi zao, jambo ambalo amesema lilimpa wakati mgumu kwani hairuhusiwi na wala haifai kununua sahihi za watu.

Kuhusu Diane Rwigara, alisema waliomsaidia kukusanya saini wanatishiwa maisha yao na watendaji wa serikali za mitaa huku wengine wamefungwa kisa walimuunga mkono anayeikosoa serikali.

Rais Kagame alikemea mwenendo wa viongozi kama hao wanaohujumu usalama wa wananchi wanaompenda mgombea fulani, akisema haifai hata kidogo na waliohusika lazima wawajibishwe.

Weka maoni