Kamata kamata ADEPR yaendelea, Askofu Rwagasana naye korokoroni

535
Askofu Tom Rwagasana ametiwa chini ya ulinzi

Naibu Msemaji wa Kanisa la Kiprotestanti nchini Rwanda, Askofu Tom Rwagasana, amekamatwa na kutiwa korokoroni na Polisi kwa kudaiwa kubadhiri mali ya kanisa hilo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, ACP Théos Badege, amesema Bishop Rwagasana alitiwa mbaroni hapo jana Jumatatu na upelelezi juu ya madai yanayomkabili unaendelea.

“Tunathibitisha utiwaji mbaroni wa Askofu Tom Rwagasana na uchunguzi wa madai ya kujilimbikizia mali katika la ADEPR unaendelea,” amesema ACP Badege.

Mchungaji huyo amefuata nyayo za viongozi wenzake watatu wanaohusika na masuala ya uchumi, ambao walitiwa nguvuni wiki iliyopita kwa kujilimbikizia mali ya kanisa hilo.

Haijajulikana ubadhirifu uliofanyika ni wa kiasi gani cha pesa ila polisi wameahidi kutoa taarifa zaidi pindi upelelezi utakapokamilishwa.

Kanisa la Kiprotestanti nchini Rwanda maarufu kama ADEPR limeshuhudia mtafaruku katika siku za nyuma, ambapo baadhi ya waumini waliutuhumu uongozi wake kwa kutumia mabavu.

Askofu Tom Rwagasana na Msemaji wa kanisa Sibomana Jean ambao ndio wapo katika nyadhifa za juu zaidi katika uongozi wa kanisa, wamekuwa wakidaiwa kuliendesha kanisa kidikteta.

‘Dove Hotel’ ya ADEPR iliyoko Jijini Kigali imehusishwa sana na madai hayo, ambapo viongozi wa dini wanadaiwa kubadhiri pesa za mkopo wa benki ambazo zilikuwa zitumike katika ujenzi wake.

Uongozi wa kanisa hili umekuwa ukitajwa kuwa baada ya kubadhiri kiasi kikubwa cha mkopo huo wa benki, waumini walishinikizwa kuchangisha pesa ya kulipa mkopo huo ili hoteli isije ikapigwa mnada.

Ni madai ambayo uongozi wa kanisa umekuwa ukiyatupilia mbali ukisema ni kweli waumini walitakiwa watoe michango yao ila walifanya hivyo kwa hiari yao na kamwe haikutumika mikwara.

Mhasibu Mkuu Sindayigaya Théophile na kiongozi anayehusika na masuala ya uchumi Mutuyemariya Christine ni miongoni mwa viongozi wa ADEPR waliotupwa lupango wiki jana.

Wazo moja

  1. Ndiyo maana sitoi sadaka tena, hawa jamaa ukitoa wanakula tu halafu wanaota vitambi kama vile vya michemsho, kuna miaka mingi nilitoa sadaka wakati sijawa na upeo mzuri wa kufikiri leo hamniwezi ng’o

Weka maoni