Kamati ya EAC yaomba Katibu Mkuu Mfumukeko atumbuliwe jipu

735
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Liberat Mfumukeko, akiongea na waandishi wa habari Arusha mwaka jana

Kamati ya Makatibu wa Kudumu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imependekeza kupigwa kalamu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Liberat Mfumukeko, wakimtuhumu kwa kuendekeza rushwa na ufujaji wa mali.

Pendekezo hilo limepitishwa baada ya makatibu hao kujiridhisha na maudhui ya ripoti mahsusi iliyowasilishwa na wakaguzi wa hesabu za jumuiya.

Ukaguzi wa mali za jumuiya hiyo umeonesha mianya ya mirungura na ufujaji wa mali, na hivyo kupelekea makatibu wa kudumu wapendekeze Mrundi Mfumukeko afukuzwe kazi.

Makatibu hao wametoa hoja ya pamoja kwamba Katibu Mkuu Liberat Mfumukeko hafai kuendelea kuiongoza jumuiya kwani ameshapoteza uaminifu.

Kikao cha makatibu wa kudumu kwa kawaida hutangulia mkutano usio wa kawaida wa baraza la mawaziri, ambapo makatibu hao hutoa ushauri kuhusu ajenda ya kikao cha marais.

Inadaiwa Mfumukeko aliuyumbisha uchumi wa jumuiya kiasi kwamba umeporomoka toka akiba ya dola miliyoni 11 Juni 30, 2016 hadi dola 19,063.

Viongozi wa EAC walikutana Arusha wikiendi hii kuzungumzia masuala mengi ikiwemo jinsi jumuiya inavyoweza kuendesha shughuli zake bila kuwategemea wafadhili.

Makatibu wa kudumu wamewataka mawaziri wawakilishi wa nchi wananachama wa jumuiya walifikishe suala zima la ufujaji wa mali ya jumuiya kwenye ajenda ya kikao cha marais ambao ndio humweka katibu mkuu wa jumuiya.

Aidha, makatibu hao wamewataka mawaziri wawachukulie hatua za kinidhamu watendaji wa jumuiya ambao wamehusika na makosa hayo ya matumizi ya ofisi, kwa ajili ya mustakbali mzuri wa jumuiya.

Chanzo: Chimp Reports

Weka maoni