Kanzu iliyojaa damu ushahidi dhidi ya mwanajeshi Rwanda kesi ya mauaji

592
Dkt Rugomwa anayetuhumiwa kwa kumuua mtoto. Ni Meja katika Jeshi la Ulinzi la Rwanda na ni daktari katika Hospitali ya Jeshi hilo.

Mahakama Kuu ya Kijeshi ya Nyamirambo inaendelea na vikao vyake vya kusikiliza kesi ya mauaji ya mtoto anayedaiwa kuuawa kinyama na Meja Dkt Rugomwa na mkubwa wake Nsanzimfura Mamarito.

Kanzu aliyokuwa amevaa Dkt Rugomwa ambaye ana cheo cha Meja katika Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) imetajwa mahakamani kama ushahidi dhidi ya mwanajeshi huyo.

Mbarushimana Théogene ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari huko Giporoso Jijini Kigali, aliuawa kwa kupigwa rungu kichwani kiasi cha kupondeka kisogo na taya la juu na vidole vyake viwili vya mkono kuvunjwa, kama inavyothibitishwa na nyaraka za uchunguzi wa madaktari, kwa mujibu wa waendesha mashtaka.

Meja Dkt Aimable Rugomwa ambaye alikuwa daktari katika Hospitali ya Jeshi la Ulinzi (RMH) iliyoko Kanombe hadi siku aliyotiwa nguvuni, anadaiwa kutekeleza mauaji hayo mnamo Septemba 4, 2016.

Waendesha mashtaka wamedai kuwa bado wanashikilia kanzu aliyokuwa amevaa Rugomwa wakati anamuua mtoto, na majibu ya vipimo vya vinasaba yameonyesha damu hiyo ni ya marehemu.

Mauaji yalifanyika nyumbani kwa Dkt Rugomwa katika Kata ya Rubiri, Tarafa ya kanombe wilayani Kicukiro, ambapo marehemu alivamiwa wakati anatoka kununua bia aina ya Primus, waendesha mashtaka wamesema.

Dkt Rugomwa akiwa na mkubwa wake walimpiga mtoto huyo na kisha kumtupa barabarani kabla ya walinda usalama kufika eneo hilo na kumwahisha hospitali, ambapo muda si mrefu alifariki dunia, kwa mujibu wa maelezo ya waendesha mashtaka.

Mashuhuda wamesema wamemuona akimpa kipigo marehemu, ambapo mkewe Uwase Scovia amewaambia waendeshaji wa mashtaka kuwa alimsihi mumewe asimuue mtu akakaidi.

Licha ya kanzu ya mshtakiwa iliyojaa damu, waendesha mashtaka wameiambia mahakama kuwa wana hata ufunguo wa magurudumu uliojipinda, na rungu waliyomuulia marehemu, vyote hivyo pia vikiwa vimejaa damu, kwa mujibu wa Izuba Rirashe.

Alipopewa nafasi ya kujitetea, Dkt Rugomwa ambaye ana cheo cha Meja katika Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) amesema tuhuma zinazomkabili hazina ukweli wowote na ushahidi uliotolewa na wanaodaiwa kuwa ni mashuhuda ni uongo mtupu.

Akielezea mazingira ya kifo cha marehemu, Dkt Rugomba ameiambia mahakama kuwa wakati anajiandaa kwenda mezani kwa ajili ya mlo, mfanyakazi wake wa nyumbani aligota mlango na kumpa taarifa ya wezi kuwavamia nyumbani ingawaje alipotoka kwenda kuwatafuta hakuwapata, na kuamua kwenda kuikongoa redio ya kwenye gari ili wasije wakaiiba.

Amesema wakati anajaribu kuikongoa redio, aliwaona watu watatu wakilisogelea gari lake huku mmoja wao akiwa na funguo, ambapo walianza kufungua magurudumu.

Amesema alitoka garini taratibu ili awakamate wezi hao ambapo walipomuona walikimbia na hapo akafanikiwa kumkamata mmoja wao, na huyo ndiye aliyepigwa mpaka kupoteza fahamu.

Mawakili wa mshukiwa wameiambia mahakama kuwa mteja wao anakiri kumpiga marehemu, ila wakaitaka isichukulie mauaji yaliyofanyika kama kitu ambacho kilikuwa kimepangwa kwani alimuua mwizi huyo katika juhudi za kujitetea kwa kuwa alikuwa amevamiwa.

Wameitaka mahakama ichukulie mauaji husika kama mauaji ambayo hayakuratibiwa.

Ombi hilo limepuuziwa mbali na waendeshaji wa mashtaka wakisema haiwezekani mauaji hayo yakachukuliwa kama kitu ambacho hakikuratibiwa ukizingatia mshtakiwa ni daktari na ni askari ulinzi ambaye anajua kuua ni kwenda kinyume cha sheria.

Mwendesha mashtaka amesema marehemu hakuwa mwizi na madai yanayohusisha wizi ni uongo uliotungwa na mshtakiwa baada ya kuona alichokifanya kimegundulika.

Kuhusu madai yanayomkabili Nsanzimfura Mamarito ambaye ni mkubwa wake na Rugomwa, mahakama imesema uchuguzi wa kitabibu kuhusu afya yake umeonesha ana matatizo ya akili na hivyo kuamua aachiwe huru kwani sheria hairuhusu kufuatilia mtu ambaye hana akili timamu.

Kesi imeahirishwa hadi Juni 6, 2017 ambapo mahakama itaendelea kusikiliza ushahidi kutoka pande zote mbili.

Weka maoni