Kesi ya askari wa Rwanda wanaoshtakiwa kwa mauaji yaendeshwa hadharani

286
Ishimwe na Nshimyumukiza baada ya kusomewa mashtaka na kujitetea

Askari wawili wa Jeshi la Ulinzi ya Rwanda (RDF) ambao ni pamoja na Ishimwe Jean Claude na Nshimyumukiza Jean Pierre wamefunguliwa mashtaka sehemu ambayo mauaji yalifanyika.

Mnamo Mei 10, 2017, askari wawili waliokuwa wakishika doria walidaiwa kumuua raia muuza baa kwa mapigo ya risasi na kusababisha kifo chake, tarafani Kagarama, mjini Kigali.

Leo hii raia kutoka huku na kule na askari ulinzi kibao wamejitokeza katika chumba cha kusikilizia kesi ambacho kwa kawaida ni ofisi ya kata ya Karugira ambayo mauaji yalitekelezwa.

Askari hao wanakabiliwa na tuhuma nyingi ikiwemo kushirikiana katika utekelezaji wa mauaji na kufyetua risasi kinyume cha sheria.

Ishimwe amekiri makosa yote huku Nshimyumukiza akikiri kosa moja tu la ushirikiano katika kuua.

Mmoja wa washukiwa wa mauaji akisomewa mashtaka mbele ya umati wa raia wa kawaida na askari wenzake waliofurika kutoka sehemu mbalimbali

Mauaji yalifanyika baada ya askari hao kuacha kazi ya doria na kuingia baa na kuwepo katika baa hiyo kwa muda wa saa nzima, kwa mujibu wa upande wa waendesha mashtaka.

Mwendesha mashtaka Cpt Ndatuhutse Rushakiro Felicien amesema kuacha kazi na kuenda baa ni kosa kwa mwanajeshi anayetakiwa awe kazini muda wa kazi, na hilo ni kosa la kukosa utiifu.

Baada ya kumuua muuza baa, askari hao walikutana njiani na raia wa kawaida na kuwauliza vitambulisho vyao kabla ya kuwapora faranga elfu 35, mwendesha mashtaka amesema.

Inadaiwa kuwa baada ya kumuua muuza baa, askari hao walimtishia maisha yake mkewe mja mzito alipowauliza ni kwa nini wanampiga risasi mumewe.

Mwendeshaji wa mashtaka amesema askari hao walimkimbiza mke huyo hadi baa jirani ambayo alikwenda kujibanza, ambapo waliharibu friji na vioo vya milango kwa risasi.

Ishimwe amesema alifyetua risasi kumtetea askari mwenzake ambaye alikuwa ananyang’anywa bunduki na marehemu, na hapo ndipo akaamua kumpiga risasi mguuni.

Kuhusu kuacha doria na kuenda baa, ametupilia mbali madai hayo akisema kwamba walishika doria kuanzia mida ya saa tisa za alasiri mpaka mida ya usiku mauaji yalipotekelezwa.

Hata hivyo, Ishimwe amekubali kuwa alikuwa amelewa lakini si katika baa hiyo.

Kuhusu pesa wanayodaiwa kumpora raia, Ishimwe amesema walipomtaka awaoneshe kitambulisho aliwakabidhi kitambulisho kikiwa kimekamatana na pesa, ambapo aliviweka mfukoni ili kumuokoa mwenzake aliyekuwa katika hatari ya kunyang’anywa bundiki na wala.

Nshimyumukiza katika kujitetea kwake, amesema aliamua kumpiga risasi mwanaume huyo akihisi kuwa ni adui kwa kuwa alimshambulia vibaya mno.

Wakili wao ameiomba mahakama iwaachie huru akiahidi kuwa hawatokwamisha juhudi za upelelezi unaondelea kuhusu makosa ya jinai yanayowakabili.

Raia wakishuhudia washukuwa wa mauaji kurudishwa kwenye gari baada ya kesi ya kusomewa mashtaka

Mahakama imesema itatoa hukumu Juni 27, 2017.

Weka maoni