Klabu ya Simba kuanza kuneemeka kupitia Pesa za Mitandaoni.

210

Kati ya klabu za Tanzania ambazo kwa siku za usoni huenda zikajivunia uwepo na ukuaji wa teknolojia, ni klabu ya Simba.Klabu hiyo kongwe, ambayo umaarufu wake ulianza mwaka 1936, huku ikiwa na wapenzi na mashabiki ndani na nje ya nchi, ina kila dalili ya kunufaika na utandawazi huo kutokana na kuanzisha APP ambayo ni maalumu kwaajili ya kutoa taarifa rasmi za klabu hiyo.

Simba inakuwa ni klabu ya kwanza nchini kufikia hatua hiyo ya kuelekea kunufaika na teknolojia kupitia APP hiyo, kutokana na namna ambavyo imepokelewa na wapenzi wa klabu hiyo mara tu baada ya kuingizwa sokoni kupitia PLAY STORE,  ikiwa ni maalumu kwa watumiaji wa vifaa vinavyotumia mfumo wa uendeshaji wa Android, huku ule wa iOS kwa maana ya watumiaji wa Apple ukiwa mbioni pia.

APP hiyo inatoa taarifa rasmi za klabu ya Simba kwa gharama nafuu, tofauti na APP nyingine zinazotumika kupasha habari mtandaoni.

Ikiwa ina muda wa miezi sita pekee tangu kuingizwa sokoni, tayari APP hiyo ambayo ipo chini ya kampuni ya EAG Group imeshushwa (Download) mara 121,000, jambo ambalo linatajwa kuwa ni ishara ya APP hiyo kufanya vizuri baadaye.

Mkurugenzi wa EAG Group, Imani Kajula, anasema kwa siku kati ya watu 1,000 hadi 2,000 wanashusha App hiyo, jambo linaloonesha dalili njema za kufanikiwa kwa APP hiyo, huku lengo likiwa ni kushushwa mara 200,000 ifikapo mwakani.

“Si uwekezaji mdogo, mpaka sasa tumetumia zaidi ya Sh milioni 400 hadi kuifikisha App hapo ilipo. Imefanyiwa kazi na watu kutoka Afrika Kusini na Israel, inahitaji uvumilivu na subira kufanya hii biashara,” anasema Kajula.

Simba App kwasasa ina kurasa nne ambazo ni Simba News inayotoa taarifa za maandishi na picha za mnato, Simba Live inayotoa matukio ya video ya timu hiyo, ambapo wameunganisha na mtandao wa Youtube na Simba Exclusive, ambapo ni maalumu kwaajili ya habari na maisha ya wachezaji na watendaji wa klabu hiyo.

APP hiyo pia iko mbioni kuanza kutoa huduma za uuzaji tiketi za klabu hiyo kwa siku za usoni, ikiwamo pia kuonyesha mechi za klabu hiyo moja kwa moja ambapo mtu mwenye APP hiyo atatakiwa kulipia Sh 1,000 pekee ili kupata uhondo huo.

APP hiyo huenda ikainufaisha zaidi klabu hiyo kutokana na kuwa na wafuasi wengi ambapo iwapo wote wataamua kuishusha kwenye simu zao, basi hakuna ubishi kwamba teknolojia itakuwa na manufaa zaidi kwa Simba.

Natumai kuwa klabu nyingine za ligi kuu Tanzania zitaiga mfumo huo ili kuweza kuvuna pesa kupitia teknolojia, mbali na kusubiri mapato ya mechi na fedha za wadhamini.

Weka maoni