Magufuli na Museveni wasaini mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta

391

Rais wa Tanzania na Rais wa Uganda, Dkt Pombe Magufuli na Yoweli Museveni, leo hii wametia saini mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania.

Wataalam wanatarajiwa kuandaa mkataba wa mradi wa Tanzania na Uganda ambao umepangwa kukamilika katika kipindi cha wiki moja, na baada ya hapo tararibu za kuweka jiwe la msingi la kuanza kwa ujenzi za mradi huo zitafanyika.

Ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,443 utagharimu dola za Marekani biliyoni 3,35 na unatarajiwa kusafirisha mapipa laki 2 ya mafuta kwa siku na ujenzi wake unatarajiwa kuzalisha ajira kati ya 6,000 na 10,000.

Rais Magufuli amemshukuru Rais Museveni kwa hatua ambayo Tanzania na Uganda zimefikia, na ameeleza kuwa mradi huo ni matokeo ya urafiki na udugu wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizi mbili.

Kwa upande wake Rais Museveni amempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa kutia msukumo mkubwa kufanikisha mradi huu na amesema mradi huu utanufaisha hasa mashirika ya ndege ambayo yatapata mafuta kwa gharama nafuu na hivyo kukua zaidi kibiashara.

Chanzo: Swahili Times

Weka maoni