Mani Martin aipongeza serikali kwa kuidhinisha Kiswahili kuwa lugha rasmi

286
Mani Martin akiimba katika tamasha la Sauti za busara mwaka 2013

Nguli wa muziki wa Rwanda Mani Martin, ameisifia Serikali ya Rwanda baada ya hatua ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi baada ya Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza.

“Nimefurahi sana kusikia serikali imeamua kukifanya kiswahili kuwa lugha rasmi, hiyo itaongeza ushirikiano kati yetu na jamii yose ya Afrika Mashariki,” amesema Mani Martin katika mazungumzo na Habari Pevu.

Msanii huyu wa ngoma za miondoko ya Afrobeat anadai ameanza kuufanyia marudio wimbo wake wa Icyo Dupfana aliouachia miaka karibia 10 iliyopita, ambapo ameutafsiri kwenda Kiswahili na utatoka siku chache zijazo.

“Nimeamua kuutafsiri kwani nimefikiria kwamba ujumbe wa amani uliomo unatakiwa ueleweke Africa Mashariki na Africa nzima,” amesema hitmaker wa Urukumbuzi, Same Room, Mazi Magari na kadhalika.

Martin ambaye amekuwa akiuwakilisha muziki wa Rwanda kwenye matamasha mbalimbali ya muziki mathalani Amani Festival huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sauti za Busara Zanzibar, amesema watu wamekuwa wakimuambia anaimba vizuri ila tatizo hawaelewi anachoimba, ndipo akafikiria kuanza kuzitafsiri nyimbo zake za Kinyarwanda hadi Kiswahili.

Amesema hajazaliwa wala kuishi kwenye jamii ya wazungumzaji wa Kiswahili ila Kiswahili ni lugha anayoipenda sana na anaiongea kwa ufasaha, hivyo hana budi kuitumia kuutangaza muziki wake kimataifa.

“Mimi Kiswahili ninachoongea nimefundishwa shuleni, lakini ni lugha ambayo naipenda sana hususan kwa muziki,” amesema Mani Martin na kuongeza kuwa Kiswahili jinsi kilivyo humsaidia kuimba kwa hisia kuliko Kifaransa na Kiingereza.

Wasifu wake

Nyota njema huonekana alfajiri. Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 6, ndipo kipaji chake kilipogundulika ambapo alikuwa anapenda kuimba darasani na kumvutia mwalimu wake.

“Mwalimu huyo alinipeleka kanisani ili kuniwezesha kuimarisha kipaji changu cha kuimba. Miaka ilikatika na ilipofika 2005 nikarekodi wimbo wangu wa kwanza Urukumbuzi uliopendwa sana nchini Rwanda na Burundi pia. Nilianza kufanya muziki kama biashara mwaka 2010 ila hapo nilikuwa tayari nimeanza kupokea tuzo tofauti ambazo ndizo zilinipa motisha.”

Miaka 12 baada ya mauaji ya halaiki dhidi ya Watutsi ilimalizika bila hata tuzo moja kutolewa kwa wasanii nchini Rwanda yamkini kwa sababu ilikuwa bado ni kipindi cha simanzi na majonzi.

Mwaka 2006 Mani Martin akawa msanii wa kwanza kutuzwa na kampuni ya Rwanda Music Promotion kwa ushirikiano wa Radio 10 kwa wimbo wake Urukumbuzi aliokuwa akitamba nao enzi hizo kabla hajateuliwa kuliwakilisha taifa lake kwenye PAM Awards mwaka uliofuatia kama msanii bora wa kiume.

Mwaka 2012 kampuni ya Ikirezi Group inayotoa tuzo kwa wasanii bora nchini Rwanda kupitia Salax Awards, ilimkabidhi tuzo ya msanii bora wa ngoma za utamaduni (Best Traditional Artist).

Kimataifa, wimbo wake My Destiny ulichaguliwa namba 14 miongoni mwa nyimbo 50 kwenye shindano la BBC World Service. Mwaka wuo huo, Mani Martin aliwakilisha Rwanda kwenye kinyang’anyiro cha mataifa watumiaji wa Kifaransa (Jeux de la Francophonie) ambapo alinyakuwa nishani ya shaba.

Bado tukiendelea kuzungumzia mafanikio ya kijana huyu kutoka nchini Rwanda, ifahamike pia kwamba kipaji chake kilimwezesha kushiriki RFI Discoveries Awards 2013 na kuja kuwa miongoni mwa wasanii kumi bora kwa Afrika Mashariki.

Alipoanza muziki, Mani Martin alikuwa msanii wa nyimbo za injili. Haikupita muda mrefu akaanza kuimba nyimbo za mapenzi na zile za kuhimiza umoja na upendo miongoni mwa Wanyarwanda, ikizingatiwa kuwa Rwanda ilighubikwa na mauaji ya kimbari yaliyosababisha mpasuko mkubwa kwenye jamii.

Weka maoni