Manusura wahuzunishwa na wauaji kukwepa vifungo Nyanza

244
Mwenge wa matumaini huwashwa kila tarehe 7 mwezi wa nne wakati wa ufunguzi wa kumbukumbu za kitaifa za mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi

Manusura wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda wametangaza kusikitishwa na kitendo cha watekelezaji wa mauaji kukwepa vifungo vyao na kutamba mitaani.

Manusura hao kutoka wilayani Nyanza katika Mkoa wa Kusini, wameeleza huzuni wanayopata wakiwaona waliowaua wanafamilia wao wakitamba mitaani bila wasiwasi wowote.

Wakati wa mauaji ya kimbari yaliyofanyika mwaka 1994 Bi Mukaniringiyimana Jeanne alikuwa na umri wa miaka 12.

Baba yake pamoja na nduguze wanne waliuawa akishuhudia kwa macho kisha wakatoswa ndani ya Mto Mumbogo.

Mwanamke huyo anaelezea kwa uchungu kisa hicho, anadai wale waliotekeleza mauaji hayo ya kinyama, siku hizi anawaona mitaani na wengine tayari wameshaungana na familia zao.

Amesema anawaona wakitamba mitaani licha ya kwamba walihukumiwa kifungo cha maisha jela kisha wakatoroka kabla ya kupelekwa gerezani.

“Huwa naumia sana rohoni pale ninapokutana nao, ninaowajua ni wengi hususani wale waliotekeleza mauaji ya familia yangu, nashangaa kuwaona wakitamba mitaani kana kwamba hakuna mabaya waliyoyafanya,” amesema Bi Mukaniringiyimana.

Inadaiwa kipindi kesi zao zinaendeshwa mahakamani, watu hao walikimbia kukwepa vifungo vyao na waliporudi nchini wakawa hawakamatwi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyanza, Mugisha Philbert, anadai kutambua tatizo hilo na kwamba tayari baadhi ya watu hao wameshakamatwa.

“Ndiyo watu hao wapo lakini wengi wao hukamatwa, mpaka sasa tunapozungumza kuna ambao wako polisi kwani ripoti zao zimejulikana,” amesema Bw Mugisha.

Kosa la mauaji ya kimbari ni miongoni mwa makosa makubwa ambayo hayazeeki, na mtu aliyehukumiwa kwa kosa hilo kisha akatoroka kifungo, hufuatiliwa hadi siku ya kifo chake.

Rwanda imekuwa ikiziomba nchi mbalimbali ziwakamate na kuwafikisha mahakamani washukiwa wa mauaji ya kimbari waliokimbilia katika baadhi ya mataifa ya Afrika, Ulaya na Amerika.

Weka maoni