Matamshi ya Magufuli yawakasirisha wanawake Tanzania

487
Rais wa Tanzania, John Magufuli

Rais wa Tanzania John Magufuli ameshutumiwa kwa matamshi yake kwamba wasichana wanaojifungua hawafai kuruhusiwa kurudi shule, kwa mujibu wa BBC.

Ombi la mitandao ya kijamii limewekwa huku shirika moja la wanawake barani Afrika likitoa hamasa ya kumtaka rais Magufuli kuomba msamaha kwa matamshi hayo.

Bwana Magufuli aliwaonya wasichana wa shule katika mkutano wa hadhara siku ya Jumatatu kwamba ”unaposhika mimba mambo yako yamekwisha.”

Magufuli amesema kuwa chini ya uongozi wake wasichana wa shule ambao hujifungua watoto hawataruhusiwa tena kurudi shuleni.

Sheria iliopitishwa mwaka 2002 inaruhusu kutimuliwa kwa wasichana waliotungwa mimba wakiwa shuleni.

Sheria hiyo inasema kuwa wasichana wanaweza kufukuzwa shuleni kwa ”makosa yanayokiuka maadili na ndoa”.

Makundi ya haki ya wanawake yamekuwa yakiishinikiza serikali kubadilisha sheria hiyo.

Magufuli ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara katika mji wa Chalinze, takriban kilomita 100 magharibi mwa mji wa Dar es Salaam alisema kuwa kina mama hao wachanga hawatasoma vyema iwapo wataruhusiwa kurudi shule.

Baada ya kupiga hesabu atamtaka mwalimu wake kwenda nje ili kunyonyesha mwanaye anayelia.

Alisema kuwa wanaume wanaouwatunga mimba wasichana wa shule pia nao wanapaswa kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 30 na kuweka nguvu zao walizozitumia kuwatunga mimba wasichana hao kulima wakiwa jela.

Nchini Tanzania kuna takriban wasichana 8,000 ambao huacha shule kila mwaka kutokana na kuwa wajawazito, kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Human Rights Watch.

Weka maoni