Mbunge Gatabazi: Sitasahau uhodari wa marehemu Mukayisenga

322
Gatabazi Jean Marie Vianney akitoa maoni bungeni.

Pamoja na kwamba baba yake na marehemu mbunge Mukayisenga Françoise alikuwa askari katika jeshi la serikali ya Juvénal Habyarimana, lakini alihamasisha amani miongoni mwa Wanyarwanda chini ya serikali ya RPF-Inkotanyi.

Haya yamesemwa na Mbunge Jean Marie Vianney Gatabazi akizungumzia alivyosikitishwa na taarifa ya kifo cha mbunge mwenzake Mukayisenga, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo.

Bw Gatabazi amesema aliporudi kutoka ukimbizini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bi Mukayisenga alijiunga na chama tawala cha RPF-Inkotanyi na kukisaidia pasipo kuchoka kufanikisha sera zake mpaka umauti ulipomvuta.

“Namfahamu vizuri sana tangu kipindi tunahudumu katika serikali za mitaa, Mukayiranga alikuwa mwanachama wa RPF-Inkotanyi aliyeonesha moyo wa kujituma, na hata aliporudi kutoka ukimbizini nchini DR Congo alipokelewa na kushughulikiwa vizuri na serikali tofauti na alivyokuwa akitarajia,” amesema.

Marehemu Mukayisenga Françoise

Marehemu Mukayisenga ni miongoni mwa Wanyarwanda walioikimbia nchi yao mwaka 1994 baada ya majeshi ya waasi wa RPA kujihakikishia udhibiti wan chi na kuyatawanya majeshi ya serikali ya kipindi hicho ambayo askari wake wengi walikimbilia nchini DR-Congo.

Kwa mujibu wa Gatabazi “marehemu Mukayisenga aliporudi nchini mwake alipewa wadhifa mzuri wakati yeye alikuwa anafikiri atafanyiwa maovu na hatathaminiwa, alishughulikiwa kwa ukarimu mpaka kupewa nafasi ya ubunge, hiyo ilimfanya apaze sauti kuzinadi sera za RPF-Inkotanyi akikitaja chama hicho kuwa ni chama kisichokuwa na ubaguzi, kinachopigania umoja wa Wanyarwanda.”

Mukayiranga alifariki dunia katika Hospitali ya Jeshi la Ulinzi ya Kanombe mjini Kigali, ambapo alikuwa amepelekwa kwa matibabu.

Haijajulikana alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa gani.

Mwanamke huyo ambaye ameiaga dunia akiwa na umri wa miaka 48, aliingia bungeni mnamo mwaka 2003 kwa tiketi ya chama cha RPF-Inkotanyi.

Weka maoni