Mbunge wa Rwanda Martin Ngoga apata dili nono FIFA

407
Mbunge Martin Ngoga

Mmoja wa wabunge wanaoiwakilisha Rwanda kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Martin Ngoga, amechaguliwa kuwa Naibu-Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya FIFA, kitengo cha upelelezi.

Matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika leo hii nchini Bahrain yametangazwa na rais wa shirikisho hilo la kimataifa la soka, Gianni Infantino.

Bw Martin Ngoga aliwahi kuwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Rwanda.

Bwana Ngoga amesema amefurahi kuaminiwa na wanasoka na yuko tayari kutoa mchango wake kupigania mustakbali mzuri wa kabumbu duniani.

Ukiacha waliochaguliwa kuingia kwenye kamati ya maadili, wamechaguliwa pia wanakamati wa kamati ya ukaguzi wa hesabu za FIFA, kamati ya uongozi na kamati ya masuala ya sheria.

Viongozi hao wameidhinishwa kwa kura 209 kati ya 211 za wawakilishi wa mashirika ya dimba ulimwenguni.

Kwa kawaida, Bw Martin Ngoga ni shabiki wa timu ya Mukura FC.

Yeye na wanakamati wenzake wamechaguliwa kuhudumu kwa mhula wa miaka minne.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili kitengo cha Upelelezi ni María Claudia Rojas kutoka Colombia. Ana manaibu wawili ambao ni Bw Ngoga na Bruno de Vita kutoka nchini Canada.

Weka maoni