Mchakato wa kupokea nyaraka za wanaotaka kugombea urais Rwanda wamalizika

452
Rais Kagame akiwasilisha nyaraka zake kwa Rais wa Tume ya taifa ya Uchaguzi profesa kalisa Mbanda Alhamisi wiki hii. Picha/Urugwiro Village.

Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Rwanda imetamatisha zoezi lililoanza tarehe 12 mwezi huu la kupokea nyaraka za maombi ya wanaotaka kuwania urais nchini humo.

Rais Kagame amekuwa wa mwisho kuwasilisha karatasi hizo Alhamisi wiki hii, baada ya kuishinishwa na chama chake cha RPF-Inkotanyi.

Washindani wake ni mwanadada Diane Rwigara, Gilbert Mwenedata, Fred Sekikubo Barafinda na Philippe Mpayimana ambao wanataka kuwania urais kama wagombea binafsi.

Ukiacha hao wagombea binafsi, yupo hata Frank Habineza aliyejipanga kupeperusha bendera ya chama pinzani alichokiasi cha Democratic Green Party of Rwanda.

Chama hicho kinachojulikana kwa ufupi kama DGPR kimekuwa chama pekee kupinga Rais Kagame kuongezewa muhula madalakani.

Rais wa NEC, Profesa Kalisa Mbanda, amesema mchakato wa kupokea nyaraka husika umefanyika katika hali ya utulivu na inaonesha upevu wa demokrasia nchini Rwanda.

Hata hivyo, Philippe Mpayimana hajaweza kupata sahihi za watu 600 anazotakiwa apate kutoka kwa wananchi ambao wanaonesha kumuunga mkono.

Wakati akiwasili katika ofisi ya NEC, alisema alipata taabu kupata sahihi hizo kwani watu walitaka awape pesa ndio wampe sahihi zao ilhali kununua sahihi ni kinyume cha sheria.

Inatarajiwa kuwa NEC itatangaza orodha ya mpito ya walioidhinishwa kugombea Juni 27.

Weka maoni