Meya mbaroni kwa kuwasumbua wagombea urais Rwanda

427
Kagame, Mpayimana na Habineza ambao wanagombea urais nchini Rwanda

Meya wa wilaya ya Rubavu Magharibi mwa Rwanda Sinamenye Jeremie na mtendaji mwingine wa wilaya hiyo wametiwa nguvuni na Jeshi na Usalama.

Wanakabiliwa na madai ya kukwamisha mipango ya wagombea urais (Frank Habineza na Philippe Mpayimana).

Msemaji wa Jeshi la Usalama ACP Theos Badege amesema viongozi hao waliwakataza raia kwenda sehemu za kampeni za wagombea hao.

Meya wa Rubavu Sinamenye Jeremie ambaye ametupwa rumande ili kupisha upelelezi juu ya madai yanayomkabili

Philippe Mpayimana mapema wiki hii alipata wakati mgumu alipoenda kupiga kampeni mjini Rubavu na kukosa watu ambapo viti vyote vilivyokuwa vimeandaliwa maalum kwa wananchi vilikuwa wazi mpaka alipoamua kuondoka.

Mpayimana alilaumu uongozi wa wilaya hiyo kwa kumuandalia sehemu ambayo haina watu wakati yeye alihitaji mahali ambapo kuna utitiri wa watu akakatazwa.

Siyo viongozi hao wa wilaya ya Rubavu ambao wamekamatwa tu kwani hata Katibu Mtendaji wa Tarafa ya Busanze wilayani Nyaruguru Kusini mwa Rwanda amekamatwa, akikabiliwa na madai kama hayo.

Msemaji wa Jeshi la Usalama ACP Theos Badege amesema viongozi hao wametupwa ndani ili kupisha juhudi za upelelezi wa makosa yanayowakabili ambao umeshaanza, na kuongeza kuwa wapo viongozi wengine wa wilaya ya Kirehe na Nyagatare Mashariki mwa Rwanda ambao na wenyewe wanachunguzwa.

Amesema kuwakataza raia kwenda sehemu za kampeni za wagombea ni uvunjifu wa sheria kwani wagombea hao wameidhinishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wananchi wana haki ya kikatiba ya kusikiliza sera za wagombea wote kabla ya kupiga kura.

Frank Habineza anayegombea kwa tiketi ya Chama cha Green Party of Rwanda majuzi alidai kukerwa na viongozi wilayani Nyagatare kumkataza kupiga kampeni sehemu aliyokuwa amepanga kisa ni karibu na soko, na badala yake kumhamishia sehemu iliyo kando ya makaburi.

Wakati matukio ya kampeni za Rais Paul Kagame yakiendelea kuvuta maelfu ya wananchi, wagombea wenza wanaendelea kupaza sauti kukemea viongozi wa serikali za mitaa kuhatarisha mipango yao kwa kuwazuia wananchi kuja kuwasikiliza.

Mgombea binafsi Philippe Mpayimana juzijuzi alikahiriwa kuondoka mbele ya Wilaya ya Nyamasheke kisa sehemu hiyo imetengwa kwa ajili ya shughuli za chama tawala.

Kampeni za urais zilianza mnamo Julai 14, ambapo wagombea ni watatu: Paul Kagame anayesaka mhula wa tatu, Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party of Rwanda na Philippe Mpayimana ambaye ni mgombea huria.

Uchaguzi utafanyika tarehe 3 mwezi kesho kwa Wanyarwanda walioko nje ya nchi na tarehe 4 kwa wale walioko nchini Rwanda.

Weka maoni