Mfungwa mtoro arudishwa Rwanda kutoka Uganda

384
Msemaji wa Jeshi la Polisi la Rwanda ACP Théos Badege (Picha/New Times)

Jeshi la Polisi la Uganda hapo jana Alhamisi lilimkabidhi kwa Polisi wa Rwanda Rugamba Jovan aliyetoroka Gereza la Nyarugenge baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji.

Bw Rugamba alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kuhusika na kifo cha Bihezande Francois mkazi wa tarafa ya Gacurabwenge wilayani Kamonyi, aliyeuawa mnamo Juni 24, 2016.

Alifua dafu kutoroka Gereza la Nyarugenge lililoko Kigali mjini kati na kukimbilia nchini Uganda na kisha kubadili majina ambapo alijiita Kaitare David kabla ya kutiwa nguvuni akiwa huko Kawempe, Kampala, kwa mujibu wa Imvaho Nshya.

Mtoro wa gereza Rugamba Jovan (wa tatu kushoto) akikabidhiwa kwa Polisi wa Rwanda hapo jana Alhamisi (Picha/Imvaho Nshya)

Msemaji wa Jeshi la Polisi la Rwanda, ACP Théos Badege, amesema polisi nchi tofauti hushirikiana hivi kwamba huwezi kufanya maovu ukakimbilia nchi nyingine usikamatwe.

“Kukabidhiwa mtoro huyu wa gereza ni ishara ya ushirikiano mwema uliopo baina ya majeshi ya polisi ya Rwanda na Uganda katika kupambana na makosa ya kuvuka mipaka,” ameongeza.

Mwaka jana Polisi wa Uganda walibrudisha Rwanda Ndimubanzi Boniface anayetuhumiwa kwa kuhusika na mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.

Mwaka mmoja kabla ya hapo, Akankwasa Brian aliyekuwa amekimbiliwa nchini Rwanda baada ya kuhusika na wizi wa shilingi miliyoni moja, alirudishwa nchini mwao na Polisi wa Rwanda.

Wazo moja

  1. Siku za mwizi ni arobaini, ila hata asingekamatwa asingekuwa na amani. Huwezi kuua mtu uwe na amani hata kama ikiendelea kuwa siri yako binafsi. Damu ni nzito kuliko maji. Mtu ambaye hujamuumba muache aishi tu hata akikuudhi vipi.

Weka maoni