Mgombea urais Rwanda Barafinda akiri kupelekwa hospitali ya magonjwa ya akili

515
Fred Sekikubo Farafinda

Barafinda Sekikubo Fred ameiteka mitandao ya kijamii nchini Rwanda baada ya jana kuibuka na kutangaza kuwa ana nia ya kuiongoza Rwanda.

Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 47 amekiri kuwa aliwahi kushughulikiwa na matabibu katika hospitali ya magonjwa ya akili ya CARAES-Ndera iliyoko mjini Kigali.

Matamshi yake yanaendelea kuwa gumzo mitandaoni ambapo baadhi wanamuita mchekeshaji asiyeweza kuongoza nchi, huku wengine wakisema kuwania urais ni haki yake ya kikatiba.

Mgombea urais mtarajiwa Fred Barafinda akiwa kwenye pozi la kustaajabisha

Jana Jumatatu ndipo alifika katika makao ya Tume Huru ya Uchaguzi (NEC) kuwasilisha maombi yake ya kugombea urais, ambapo hapo ndipo maneno ya kejeli dhidi yake yakaanza.

Barafinda (kushoto) akitafuta nyaraka kwenye begi lake katika chumba cha Tume Huru ya Uchaguzi. Ambaye amekaa kulia ni Rais wa tume hiyo, Profesa Kalisa Mbanda.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kwa nini anataka kuwa rais wa Rwanda mara baada ya kukutana na viongozi wa Tume Huru ya Uchaguzi, alitoa majibu haya: “Sababu ni homoni za kisiasa nilizo nazo tangu utotoni, leo kutaka kugombea urais siyo ajali, hivi karibuni mtampata mwanasiasa mahiri.”

Barafinda amesema ana watoto kumi aliozaa na mke mmoja, ambapo katika watoto hao mkubwa ana umri wa miaka 19. Amesema ataendelea kuzaa kwa misingi kwamba uchumi wa nchi ni raia.

“Bibi yangu alizaa watoto 25, mama kazaa 20 mimi ndio nimefikisha 10, uchumi wa nchi ni raia wake, si ndiyo? Au unadhani ni ardhi tu? Angalia nji jirani watu wanazaa watoto wengi kuliko sisi ndiyo maana wametufunika kiuchumi,” amesema mgombea urais mtarajiwa.

Matamshi ya Barafinda yanaonekana kukinzana na sera ya serikali ya uzazi wa mpango ambapo wananchi wamekuwa wakihamasishwa kuzaa watoto wachache wanaoweza kuwatunza.

Bw Barafinda amesema pia aliwahi kupekelekwa hospitalini CARAES-Ndera kwa matibabu ya mapungufu ya akili ila vidonge alivyopewa aligoma kuvinywa kwani alijua hana tatizo lolote.

“Akili yangu ndio iliniponza, watu walinilia njama kutokana na akili yangu ambapo wanatamani kichwa changu kingekuwa chao. Ndiyo maana dawa hizo sikuzitumia kwani sikuwa mgonjwa. Leo sinywi hizo dawa unaona nina tatizo? Ninawaongoza vizuri wanachama wangu ambao ni zaidi ya miliyoni 9,” amesema Barafinda kwa mujibu wa Ukwezi.com

Alipoulizwa kuhusu uzoefu wake katika masuala ya uongozi, amesema hahitaji uzoeufi mwingine kwa kuwa ana akili ya kutosha inayomwezesha kuvuka barabara bila kugongwa na magari na anaamimi kwa kutumia akili yake hiyo anaweza kuongoza hata dunia.

Amewashangaza watu kwa kusema kuwa ana chama kiitwacho RRUDA (Rwanda Revolutionary Union Democratic Advancers) hakijasajiliwa rasmi, akisema chama hicho kina wanachama miliyoni 9,8.

Amesema anaamini Wanyarwanda watampa kura zao katika uchaguzi mkuu wa urais unaotarajiwa kufanyika mnamo Agosti 3-4, 2017 kwani ana sera nzuri alizozitaja kuwa ni 200.

Idadi ya wanachama cha RUDA imezua maneno mengi mitandaoni huku baadhi wakijiuliza ni vipi chama kitakuwa na wanachama wengi kihivyo wakati Rwanda nzima ina raia wasiozidi miliyoni 12.

Sensa ya mwaka 2012 iliyofanywa na Taasisi ya Takwimu nchini Rwanda (NISR) ilionesha Rwanda ina raia miliyoni 10,5 ambao zaidi ya miliyoni tano wana wana umri wa miaka chini ya 19.

Huku wagombea urais wengine wakitakiwa na NEC kukusanya sahihi za wananchi angalau 600 wanaothibitisha kuwaunga mkono ili maombi yao ya kugombea urais yaweze kubarikiwa, mwanaume huyo amesema yeye hana mpango wa kuenda mikoani kutafuta watu wa kumpa sahihi zao, akisema ana uhakika watu wenyewe watamfuata nyumbani kwake anakoishi tarafani Kanombe jijini Kigali kwani sera zake zinajinadi zenyewe.

Amesema kama atachaguliwa kuwa rais atafuta kodi za ardhi na makazi kwani ardhi na makazi ni vitu ambavyo wanyarwanda walijaaliwa tangu miaka ya zamani na hivyo haoni sababu ya serikali kuwatoza watu kodi hizo.

Alipoulizwa kuhusu elimu yake, ametoa jibu ambalo liliwafanya waandishi wa habari waangue kicheo: “Umri wa miaka 47 nilio nao ni elimu tosha kwani hata ambaye ana shahada ya uzamivu kutoka Harvard University hawezi kunyeshesha mvua.”

Chama cha PL chafuata nyayo za PSD kumuunga mkono Kagame uchaguzi

Weka maoni