Mke amuua mumewe kwa jembe na kumzika chumbani Nyabihu

607

Mwananke mkazi wa Kata ya Gisizi, Tarafa ya Jomba, Wilaya ya Nyabihu Magharibi mwa Rwanda, amemuua mumewe kwa jembe na kumzika ndani ya nyumba yao.

Inadaiwa marehemu alipigwa jembe upande wa kisogo na upande wa paji la uso pia kabla ya kufukiwa kwenye shimo chumbani.

Umuseke wanadai mwanamke huyo aitwaye Charlotte Mbarushimana, 22, alimuua Theoneste Twahirwa, 25, ikiwa ni siku ya Alhamisi Mei 11, 2017, na kisha kurudi kwa wazazi wake.

Maiti ya marehemu iligundulika ikiwa katika shimo ilimofukiwa huku juu yake yakiwa yamewekwa majani ya migomba, kwa mujibu wa maelezo ya jirani yake.

Kutokana na udogo wa shimo hilo, ilibidi miguu ya marehemu ipindwapindwe.

Siku ya kifo cha marehemu, alikuwa amerudi kumtembelea mkewe huyo ambaye alikuwa amemtelekeza baada ya kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na hawara mwingine.

Kabla hajamtelekeza, walikuwa wamejaaliwa kupata mtoto mmoja ambaye aliendelea kulelewa na mama yake.

Alipofika nyumbani kwa wazazi wake baada ya kutekeleza mauaji hayo, aliomba msaada wa kufikishwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ombi lake hilo liligonga mwamba ambapo wazazi wake walitoa taarifa polisi kuhusu mauaji yaliyofanywa na mwanao na azma aliyokuwa nayo ya kukimbilia nchini Congo.

Bi Mbarushimana alitiwa mbaroni hapo jana Jumatatu na Jeshi la Polisi ambapo anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Jomba.

Katibu Mtendaji wa Tarafa ya Jomba Albert Musirikare amesema taarifa zilizotolewa na majirani zinaeleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni marehemu kutangamana na kimada.

Inadaiwa Tarafa hiyo ya Jomba inashuhudia idadi kubwa ya wanaume ambao wana vimada, hali inayosababisha mauaji ya mara kwa mara yatekelezwayo na wanawake kutokana na wivu.

Maiti ma marehemu ilikuja kufukuliwa kwa ajili ya kuhamishiwa makaburini Mei, 14, 2017.

Weka maoni