Mkombozi afunguka kuhusu wimbo wake wa ‘Mwana w’u Rwanda’ uliokosa promo

414
Nzeyimana Thomas almaarufu Mkombozi, nguli wa muziki wa Rap kutoka Burundi ambaye anaishi Kigali kama mkimbizi (Picha/Buja Today)

Mnamo Julai 2016 ndipo msanii wa Kirundi Nzeyimana Thomas maarufu kama Mkombozi alipokimbia machafuko ya kisiasa yaliyokuwa yakilitikisa taifa lake la Burundi.

Alipofika Rwanda rapa huyu alitoa nyimbo mbili ambazo ni pamoja na ‘Ibaze nawe’ aliomshirikisha Uncle Austin na Mwana w’u Rwanda akiwa na watoto kwenye kibwagizo.

Habari Pevu tumemtafuta kutaka kujua hasa lilipotoka wazo la kutunga Mwana w’u Rwanda, wimbo unaohamasisha amani na upendo miongoni mwa Wanyarwanda.

“Kuna mtoto mdogo wa kike alikuwa anapenda kuja kwangu, mtoto wa jirani, akawa ananipenda sana mpaka akiwa nyumbani kwao analia anataka kuniona mimi, anaitwa La Douce. Huyo mtoto nikasema nitatunga wimbo wa kumsifia niuite Mwana, baadaye ndo nikafikiria eti kwa nini nisiufanye uwe kitu kikubwa, niwaimbie vijana wote wa Rwanda nikihamasisha upendo?”

Mkombozi amesema hapo ndipo alipoanza kuandika mistari kuhusu Wanyarwanda kwa ujumla, akisisitiza umuhimu wa vijana wa Rwanda kufuata nyayo za wazazi wao kulijenga taifa ambalo miaka ya nyuma liliyumba hasa kutokana na mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.

Hata hivyo Mkombozi anadai wimbo huo haujafanya vizuri kama alivyotegemea, ambapo anahisi ilitokana na kipindi ambacho aliutoa, ambacho ni muda kidogo kabla ya kumbukumbu za mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi ambapo shughuli za burudani huwa haziruhusiwi nchini Rwanda.

“Huu ndio wimbo ambao nilidhani Wanyarwanda wataupenda sana kwani nimewaimbia wao, hata mimi ndio wimbo ambao naupenda sana kati ya nyimbo zangu, ila cha kushangaza watu hawajahamasika, nadhani ilitokana na Cyunamo (kipindi cha kumbukumbu za mauaji ya kimbari), nina imani sasa watu wataupenda yaani sijakata tamaa.”

Amesema kuna nyimbo nyingi alizotoa za kuhimiza undugu na mshikamano miongoni mwa Warundi, na safari hii akaamua kuimba kwa ajili ya Wanyarwanda ambao “kusema kweli walifanya vitu vingi mpaka kulifikisha taifa hapa lilipo.”

Aidha Mkombozi amewataka Warundi waliomrushia maneno ya sumu mitandaoni wakihoji ni kwa nini akatunga wimbo wa kuisifia Rwanda wakati anajua nchi hiyo na Burundi haziivi, ambapo amewataka waelewe kwamba yeye siyo msaliti kama baadhi yao wanavyomchukulia.

“Kwenye mitandao ya kijamii naona wengine wananiponda ila ukweli ni kwamba mimi napenda amani na siyo Warundi tu nawatakia amani na nimewaimbia nyimbo kibao, nataka amani duniani kote, ndiyo maana nikawapongeza Wanyarwanda, hayo masuala mengine ya kisiasa eti mimi msaliti hayafai hata kidogo ila naamini watabadilika, ipo siku watanielewa.”

Mariya Yohani na Aline Gahongayire ndio wasanii wa Rwanda ambao Mkombozi ana ndoto za kufanya nao kazi.

Mkombozi aliingia kwenye ramani ya muziki mnamo mwaka 2008 ambapo aliwateka Warundi wengi kwa nyimbo zake, ambapo zipo hata zinazoiponda Serikali ya Rais Nkurunziza.

Ukitaka kuzungumzia nyimbo zake alizowashirikisha wasanii wa mataifa mengine, huwezi kusahau kuutaja East Africa aliomshirikisha Ali Kiba kutoka Tanzania miaka ya nyuma.

Wazo moja

  1. Mkombozi chapa kazi bhana achana na wanaokuita wasaliti, hao wasikukwamishe, nimeupenda sana huo wimbo wako wa Mwana w’u gwanda, ni mzuri sana una ujumbe mzuri. Hao warundi wengine waache waongee wakichoka midomo wataifunga.

Weka maoni