Mmiliki wa Alibaba kuanzisha miradi kabambe ya kuwanufaisha Waafrika

212
Jack Ma akiongea kwenye mkutano wa YouthConnekt Afrika unaoendelea mjini Kigali

Mkurugenzi Mkuu Mtendaji (CEO) wa kampuni kubwa ijishughulishayo na biashara ya mtandaoni (e-commerce) nchini China, Jack Ma, amesema yuko tayari kuwasaidia Waafrika.

Biliyonea huyo ambaye ndiye tajiri namba mosi barani Asia na tajiri namba 14 duniani kote, yupo nchini Rwanda katika kikao kinachoendelea cha YouthConnekt Summit.

Siku ya leo (Ijumaa), wakati akiongea kwenye kikao chake, alichukua mikrofoni na kutangaza mpango wake wa kuanzisha miradi minne mikubwa inayolenga kuwanufaisha Waafrika.

Amesema miradi hiyo bila shaka itawawezesha wajasiriamali wa kiafrika kujiendeleza na hivyo kuchangia kuimarisha uchumi wa nchi zao, kwa mujibu wa KTPress.

Katika mradi wa kwanza, Jack Ma amewaalika vijana 200 wajasiriamali kutoka Afrika kuja kufanya kazi katika kampuni yake ya Alibaba katika sekta ya e-commerce na wavuti.

“Watarudi Afrika kuendeleza biashara zao binafsi na kuwasaidia wenzao kukuza biashara zao pia,” amesema Jack Ma, akieleza umuhimu wa mradi wake huo wa kwanza.

Jack Ma akiongea kwenye kikao pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame mjini Kigali. Picha/KTPress.

Kuhusu mradi wa pili, raia huyu wa Uchina amesema atashirikiana na vyuo vikuu vya Afrika na serikali barani huyu kuharakisha maendeleo ya wavuti na biashara ya mtandaoni pia.

Mradi wa tatu utahusisha Paradise Foundation of china ambapo utalenga ukuzaji wa juhudi za utunzaji wa mazingira barani Afrika, hasa usalama wa ndovu na wanyamapori wengine.

“Tutatoa tuzo kwa watunza wanyama kwa miaka kumi ijayo kuwashukuru kwa jitihada zao za kulinda mazingira,” ameongeza Jack Ma.

Akielezea mradi wan ne, tajiri huyo amesema anataka kuonesha ni jinsi gani anavyothamini Afrika na katika mantiki hiyo atawekeza katika vijana wa bara hili.

“Nitaanza na mfuko wa kuwasaidia wajasiriamali wa kiafrika ili watimize ndoto zao,” amesema Jack Ma ambaye ana umri wa miaka 53.

Amesema atawekeza kitita cha dola 10 bilioni katika mfuko huo, na kuongeza, “naamini watu wengine wataudhamini mfuko huo pia na kuufanya uwe mpana zaidi.”

Alibaba Group Holding Limited ni kampuni kubwa ya biashara ya mtandaoni ambayo ilianzishwa na Jack Ma mnamo mwaka 1999 baada ya kuzindua tovuti ya Alibaba.com

Mtaji wa Alibaba ni dola 231 miliyoni.

Weka maoni