Mnyarwanda kufurushwa Denmark kwa mauaji ya kimbari

442
Mwenge wa matumaini huwashwa kila tarehe 7 mwezi wa nne ambapo huanza maadhimisho ya kitaifa ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi

Mnyarwanda anayedaiwa kuwa mfanyakazi wa kampuni ya teknolojia huko Denmark, anatarajiwa kurudishwa Rwanda ambapo anatuhumiwa kwa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.

Waendesha mashtaka wa Denmark wamesema mwanaume huyo ambaye ana umri wa miaka 49 anashtakiwa kwa kuhusika na mauaji ya Watutsi zaidi ya elfu moja.

Mwanaume huyo ambaye inadaiwa anaitwa Wenceslas Twagirayezu, alipata uraia wa Denmark mnamo mwaka 2004 ikiwa ni baada ya miaka mitatu akiishi nchini humo.

Mwendesha mashtaka mkuu wa Rwanda, Jean Bosco Mutangana amesema hajajua chochote kuhusu Bw Tugireyezu kurudishwa Rwanda, lakini Rwanda ilitoa hati ya kumakatwa kwake.

Imeripotiwa mshukiwa huyu ambaye anaongoza shirika la Dutabarane Foundation nchini Denmark, alikuwa mwalimu wa shule ya sekondari wilayani Rubavu wakati wa mauaji husika.

Bw Mutangana amesema mstakiwa huyo alikuwa Mwenyekiti wa chama cha CDR katika tarafa moja ya wilaya ya Rubavu, na alijulikana kama kiongozi genge la wauaji wilayani humo.

Chama cha CDR kilihusika sana katika utekelezaji wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyogharimu maisha ya watu zaidi ya miliyoni moja katika kipindi cha miezi mitatu tu.

Endapo Tugireyezu atarudishwa Rwanda, atakuwa mtu wa pili kufurushwa na taifa hilo la Ulaya Kaskazini baada ya Emmanuel Mbarushimana aliyepaishwa ndege mnamo mwaka 2014.

“Denmark ni nchi ambayo tumekuwa tukishirikiana vizuri katika mchakato wa uwajibishwaji wa wale waliohusika na mauaji ya kimbari, naamini hata safari hii mambo yatanyooka,” amesema Mutangana Jean Bosco.

Mbarushimana aliyerudishwa nchini Rwanda miaka mitatu iliyopita, kesi yake imeanza kusikilizwa ambapo anatuhumiwa kwa kuratibu mauaji ya kimbari wilayani Gisagara.

Kipindi cha mauaji hayo alikuwa ni Mkaguzi wa Elimu katika wilaya ya Muganza.

Chanzo: The New Times

Weka maoni