Munyagishari ahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya kimbari

126
Munyagishari (aliyefungwa mapingu mikononi) katika uwanja wa ndege wa Kigali akitokea Arusha, Tanzania, Julai 23, 2013

Mahakama Kuu nchini Rwanda imemhukumia kifungo cha maisha gerezani Bernard Munyagishari baada ya kumtia hatiani kwa kuhusika na mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.

Akisoma hukumu leo tarehe Aprili 20, hakimu amesema Munyagishari amekutwa na makosa mawili kati ya matano yaliyokuwa yanamkabili.

Mahakama imemtia hatiani kwa kosa la kushiriki katika mauaji ya kimbari, na hatia ya kuua kama kosa la uhalifu wa kibinadamu.

Bw Munyagishari,57, alikabidhiwa kwa Rwanda na Mahakama ya ICTR iliyoko Arusha Tanzania, mnamo Julai 2013 ili kesi yake iendeshewe nchini Rwanda.

Mahakama imesema haikujirishisha na ushahidi uliotolewa na waendesha mashtaka kuhusu kosa la ubakaji wa wanawake ambalo lilikuwa linamkabili Munyagishari.

Munyagishari alikuwa mfanyakazi katika ofisi ya katibu wa MRND, chama tawala cha miaka hiyo,  na alishiriki katika mikutano ya maandalizi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi, kwa mujibu wa mahakama.

Mahakama imesema imeridhika na ushahidi wa utetezi uhusuo Munyagishari kula njama za mauaji na kuwapa wanamgambo wa Interahamwe mafunzo ya kuwaua Watutsi.

Mahakama imesema ushahidi wa aliyedai kupewa na Munyagishari mafunzo ya kuua Watutsi ambayo vijana wa Interahamwe walikuwa wanapewa kila Jumatatu na Jumamosi katika Uwanja wa Soka wa Umuganda, ni ukweli.

Zimetajwa pia orosha za majina ya Watutsi zilizofanywa kurahisisha mauaji yao, jumbe za chuki zilizosambazwa, vizuizi vilivyowekwa barabarani na silaha kutoka Kigali zilizotumika kuulia Watutsi, ikidaiwa kuwa Munyagishari alihusika na utoaji wake.

Mahakama imesema ushahidi huo ni wa kuaminika na ni ishara kwamba mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliratibiwa.

Akisoma hukumu, hakimu amesema makosa aliyoyafanya Munyagishari yanaonyesha ukatili wa hali ya juu, ambapo yalisababisha mtafaruku kwenye jamii ilhali mtuhumiwa alikuwa ni msomi.

Katika mchakato wa uendeshaji kesi, mshukiwa aliwakataa mawakili aliopewa ambao ni pamoja na Bikotwa Bruce na Umutesi Jeanne d’Arc, ila waliendelea kumwakilisha kutokana na mahakama kutoridhika na sababu zake za kutokuwa na imani nao.

Baada ya hakimu kutoa hukumu leo, mawakili wa mshtakiwa wamesema wanapinga hukumu hiyo na wanakata rufaa, ambapo wamedai wataweka bayana dosari walizoziona wakishapata nakala ya hukumu.

Weka maoni