Waziri Mushikiwabo na RURA waikosoa NEC kuzima mitandao ya kijamii

402
Waziri wa mashauriano ya kigeni na msemaji wa Serikali ya Rwanda, Bi Louise Mushikiwabo (Picha/New Times)

Mamlaka ya Mawasiliano nchini Rwanda (RURA) imeukosoa uamuzi uliotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi (NEC) kuhusu mpango wa kuizima mitandao ya kijamii katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa rais.

Mei 29, 2017, Rais wa NEC, Profesa Charles Mbanda, alisema wanafikiria kuhusu kuifungia mitandao ya kijamii kipindi cha uchaguzi mkuu unaokaribia ili isije ikatumiwa vibaya.

Tamko hilo la NEC lilikemewa vikali na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wakisema hatua hiyo inalenga kuwanyamazisha wapinzani.

Mwenyekiti wa Chama cha upinzani cha Democratic Green Party of Rwanda, Frank Habineza, alisema hatua hiyo ni ya kuchukiza na anajiandaa kuishtaki NEC.

RURA, kupitia msemaji wake Anthony Kulamba, leo Jumatano imewatuliza wananchi kwa kusema kuwa NEC haina haki ya kudhibiti matumizi ya mitandao.

Anthony Kulamba amesema RURA ndiyo inahusika na udhibiti wa huduma za mawasiliano na siyo NEC. Bonyeza hapa kupakua tangazo la RURA kwa umma.

RURA imesema haijaongea chochote na NEC kuhusu ulazima wa kuifungia mitandao ya kijamii.

Waziri wa mambo ya nje ya nchi , Bi Louise Mushikiwabo, amekemea uamuzi huo wa NEC akisema Wanyarwanda hawatakiwi kunyimwa uhuru wa kutoa maoni yao.

Katika tamko la hapo awali, Professa Charles Mbanda alisema NEC itahitaji kuchunguza jumbe za wagombea urais kabla hawajazirusha mitandaoni.

Profesa Mbanda alisema mgombea atakayekaidi agizo hilo atachukuliwa hatua.

Waziri Mushikiwabo ambaye ndiye msemaji wa serikali, amesema Wanyarwanda wanahitaji uhuru wa kujieleza na maudhui ya jumbe zao hayatakiwi kuchunguzwa namna hiyo.

Uchaguzi wa mkuu wa rais nchini Rwanda unatarajiwa kufanyika Agosti 3-4, 2017.

Ghana na Uganda ni miongoni mwa nchi ambazo ziliizima mitandao ya kijamii katika kipindi cha uchaguzi wa rais.

 

Wazo moja

  1. Nimefurahi kusikia tamko hilo na RURA, kwa kweli dunia hii inahitaji maoni ya watu tofauti na Rwanda itajengwa na misingi ya maoni tofauti siyo NEC inachunguza maudhui ya messages za watu kabla hawajaziposti. Shukrani kwa wanaohusika kwa kuizomea NEC mmefanya kitu cha maana

Weka maoni