Nitatoboa Afrika Mashariki kupitia mgongo wa The Ben – Kid Gaju

244
Kid Gaju (nyuma) na The Ben wakiutambulisha wimbo wao wa kushirikiana

Huku baadhi ya wadau wa muziki wakidai hakuna msanii wa Rwanda ambaye ni nyota ya kimataifa, Kid Gaju hakubaliani nao na anaamini wimbo aliomshirikisha The Ben majuzi utamfikisha mbali.

Wimbo huo wa Kami ambao ulitengenezwa nchini Uganda, Kid Gaju anasema aliamua kumshirikisha The Ben katika juhudi za kutafuta tobo la kuingia Afrika Mashariki kwani “The Ben tayari ni staa”

“Nataka nifike mbali na The Ben ni gwiji, ana umaarufu katika eneo la Afrika Mashariki, ni miongoni mwa wasanii walio mstari wa mbele kwa Afrika Mashariki, hata wakati tunafanya huo wimbo tulikuwa tunatoka kwenye tamasha lake lililofanyika huko Uganda na halijahudhuriwa na Wanyarwanda tu na lilikuwa na msisimko,” amesema Kid Gaju katika mahojiano na Habari Pevu.

Alipoulizwa anavyolichukulia jina lake kwenye ramani ya muziki kwa Afrika Mashariki, Muhinyuza Justin almaarufu kama Kid Gaju amesema watu wanamjua ila anajua safari bado ndefu na ndiyo maana akaamua kufanya wimbo wa kushirikiana na msanii ambaye anaamini atampandisha hadhi.

Kwa sasa The Ben yuko Marekani ambako amekuwa akiishi tangu mwaka 2010. Kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, amesema ana amini huu wimbo utamsaidia Kid Gaju kufika mbali kumuziki.

The Ben na Meddy watakuwa ndiyo wasanii wa Rwanda ambao wanaongoza kwa kuwa na mashabiki wengi japokuwa hakuna takwimu za kuthibitisha hilo.

Wawili hao ambao wanajikita kwenye muziki wa mapenzi wa miondoko ya RnB, walikwenda Marekani miaka saba iliyopita ambapo The Ben alirudi kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka jana kwa ajili ya tamasha la The East African Party, huku Meddy mashabiki wake wakiwa hawajamweka machoni kuanzia alipoondoka ukiacha tu kupitia video anazoachia.

Katika tamasha hilo la The East African Party ambalo hufanyika kila tarehe mosi mwezi wa kwanza, The Ben alitumbuiza kwa muda wa masaa mawili bila kumpumzika wala kunywa maji, ambapo aliwaacha hoi mashabiki wake waliokuwa wakiimba naye kwa kuwa nyimbo zake takribani zote kama Habibi, I am in love na zingine wamezikariri.

Kid Gaju ana imani atafika sehemu nzuri kwenye ulingo wa muziki Afrika Mashariki kupitia wimbo huo aliomshirikisha The Ben.

Kufikia leo Kid Gaju ameachia santuri moja yenye nyimbo 12 zikiwemo Gahunda (mpango) aliomshirikisha Cindy wa Uganda, Ndakurwaye (wewe ndio gonjwa langu) aliowashirikisha Dream Boys, Mama Bebe, Njyenyine (Peke yangu) na nyinginezo nyingi.

Wimbo wake mpya wa Kami ndio wa kwanza kwenye santuri yake ya pili ambayo anadai ameanza kuikalia kitako.

Wazo moja

  1. Huyu Kid hajui anachosema, tangu lini The Ben akawa staa East Africa? The Ben hajulikani Kenya hajulikani Tanzania Uganda ndo sijui, ila ukiwataja wasanii 50 bora kwa Afrika Mashariki hawezi kuwemo. Hata yeye ni staa wa rwanda tu hajawazidi wengine. Ana kipaji ila wanyarwanda tu ndo wanajua hilo. Sasa huyu Kid sijui anaongea vitu gani au mwandishi amemsingizia? Alichoongea kinaonyesha kweli ni kid hajawa mtu mzima

Weka maoni