Pikipiki zilizotengenezwa Rwanda kuingia sokoni mwezi huu

1046
Hii ni miongoni mwa pikipiki zilizotengenezwa na kampuni ya RMC

Kampuni ya utengenezaji pikipiki ya ‘Rwanda Motorcycle Company’ (RMC) inatarajia kuanza kuuza pikipiki ilizotengenezea nchini Rwanda mwezi huu.

Kampuni hii yenye mtaji wa dola za kimarekani miliyoni moja na laki mbili ($M1,2) huendeshea shughuli zake katika eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanda la Kigali Special Economic Zone.

Uongozi wa kiwanda hiki umesema umeiunga mkono serikali katika kampeni ya Made in Rwanda inayolenga kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini Rwanda.

Pikipiki hizo huzalishwa kutokana na vyuma vinavyoagizwa kutoka Uchina ila RMC wamesema wamejipanga kuanza kununua vyuma vinavyotengenezwa nchini Rwanda.

McPhee Christopher ambaye ndiye kiongozi wa RMC amebainisha kuwa pikipiki zao zilizotengenezwa mjini Kigali zitaingia sokoni tayari kununuliwa mnamo wiki mbili zijazo.

“Wiki mbili zijazo tutazindua pikipiki hizo, tumeanza na pikipiki za usafiri wa abiria,” Bw McPhee amesema.

Kiongozi huyu ameongeza kuwa baada ya pikipiki hizo za abiria, zitafuata pikipiki maalum kwa walinda amani wakiwemo askari polisi na askari wa jeshi la ulinzi.

Mwekezaji huyu ambaye ni raia wa Marekani amesema ameamua kuja nchini Rwanda baada ya kufanya upembuzi yakinifu wa mazingira ya uwekezaji nchini humu na kuyapenda.

Amesema kwa sasa wanatengeneza pikipiki 130 kwa mwezi ila lengo ni kutengeneza idadi hiyo kwa wiki kuanzia miezi sita ijayo.

Wiki iliyopita wanafunzi 12 wa Chuo Kikuu cha Singhad Technical Education Society – Rwanda (STES-Rwanda) walizindua gari linalotumia nishati ya mionzi ya jua.

Wazo moja

  1. Serikali iwasaidie na wajasiriamali wa kinyarwanda itasaidia kuharakisha maendeleo. Tunapoteza kiasi kikubwa cha pesa kuagiza magari kutoka nchi za nje, tunakuza uchumi wao wakati wa kwetu unayumba, kwa hiyo tuvipende vitu vya kwetu tukazane mpaka tuwe na viwanda vingi huku kwetu.

Weka maoni