Pilato akanusha kuukopi wimbo wa Nitarejea wa Diamond, adai haogopi kushtakiwa

418
Diamond na Pilato

Pamoja na kwamba wimbo wa Nzagaruka umeshabihiana na wimbo wa Nitarejea wa Diamond Platnumz, msanii Pilato amesema hajaukopi wimbo huo wa Diamond na wala haufahamu.

Ukiacha mtindo na lugha, nyimbo hizo zimefanana kimaudhui toka mwanzo mpaka mwisho. Lakini Pilato akizungumza na Habari Pevu, amesema huo wimbo alijitungia yeye mwenyewe.

“Diamond namfahamu lakini huo wimbo siufahamu,” amesema Pilato na kuongeza kuwa hata hivyo wasanii wanaweza kuimba kuhusu mada moja hivyo haoni kinachowashangaza watu.

“Professa Jay kaimba ‘Piga makofi’ na Sean Paul kaimba ‘Clap’ yaani wanamuziki wote wana aidea moja, hiyi nyimbo ya Diamond siifahamu japo wengi waliniambia eti nimekopi wimbo wa Diamond nikawaambia hamna. Juzi kuna mtangazaji kaniambia ‘hii nyimbo ni ya Diamond bhana’ nikamuambia ‘mimi sijui’,” ameongeza Pilato ambaye anafanya muziki wa ‘Katuni Style’

Pilato amesema amezipata taarifa kutoka kwamba Diamond amesema atakuja nchini Rwanda kudai haki yake kama mmiliki wa hatimiliki, jambo ambalo Pilato amesema halimtishi hata kidogo kwani anajua hajafanya wizi wowote.

Alipoulizwa kama hana hofu ya kupandishwa kizimbani kwa mashtaka ya uvunjivu wa hatimiliki, Pilato ametoa majibu haya: “Siwezi kuingia matatani ndugu yangu, nyimbo yake siifahamu, siwezi kuchukua nyimbo yake niibadili kwa Kinyarwanda…”

Aidha, Pilato amesema hata kumkubali Diamond hamkubali, akisema msanii ambaye anamtazamia ni Yousou Ndulu kutoka nchini Senegal.

Weka maoni