Polisi wa Rwanda wavishwa nishani Haiti

201
Polisi wa Rwanda wakivishwa nishati Haiti wikiendi iliyopita

Umoja wa Mataifa wikiendi iliyopita uliwavisha nishani maafisa 8 wa Jeshi la Polisi la Rwanda walio katika operesheni ya urejeshaji amani nchini Haiti kwa kuchapa kazi kiueledi.

Katika sherehe za kuwavisha nishani ziliyofanyika Port Au Prince, Naibu-Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Moustafa Benlamlin, aliwapongeza polisi wa Rwanda.

Moustafa Benlamlin alisema amefurahishwa na umahiri na nidhani vya Polisi wa Rwanda walio nchini humo katika operesheni ya Umoja wa Mataifa ijulikanayo kwa ufupi kama MINUSTAH.

“Mmefanya kazi kwa heshima, mmejitolea, mmetumia bidii na hiyo ndiyo hadhi yetu kama Umoja wa Mataifa,” alisema Benlamlin katika kilele cha sherehe za utoaji nishani.

Aidha Benlamlin amewashukuru Polisi wa Rwanda kwa juhudi zao katika kufunza ngazi za usalama nchini humo, ambapo alidai wamechakarika kuliko walivyotarajiwa.

Kamishna wa Polisi wa MINUSTAH, Brig Jen Monchotte, amesema “Polisi wa Rwanda wamekuwa wakishiriki katika operesheni za kurudisha amani sehemu nyingi duniani. Wamekuwa sehemu ya MINUSTAH tangu 2010, mmeonyesha uhodari katika kulijenga Jeshi la Polisi la Haiti.”

Amekumbushia kuwa “Rwanda ni mdau muhimu wa Umoja wa Mataifa katika jitihada za kusaka amani,” ambapo ina jumla ya walinda amani elfu 6 wakiwemo na askari magereza.

Picha ya kumbukumbu baada ya kuvishwa nishani

Idadi ya maafisa wa Jeshi la Polisi la Rwanda walio nchini Haiti ni 178.

“Nataka niwakumbushe kuwa kama watangulizi wenu, mmetoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Jeshi la Polisi la Haiti kuhakikisha kunakuwepo na mazingira mazuri ya amani na utulivu,” alisema Brigedia Jenerali Monchotte.

Akiongea kwa niaba ya waliovishwa nishani, Supt. Eric Murenzi ameelezea msimamo wa Rwanda katika harakati za kujenga amani, na kuushukuru uongozi wa MINUSTAH kwa ushirikiano imara katika kutimiza majukumu katika viwango vya Umoja wa Mataifa.

Weka maoni