Polisi wamuua kwa risasi aliyempiga upanga DASSO Rusizi

212
Msemaji wa Jeshi la Polisi la Rwanda, ACP Théos Badege

Namahoro Jean Bosco, 27, aliyekuwa akishikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kamembe Wilayani Rusizi nchini Rwanda ameuawa kwa mapigo ya risasi masaa machache baada ya kutiwa nguvuni.

Mauaji yake yalifanyika tarehe Aprili 20, 2017 wakati “akijaribu kutimua mbio,” kwa mujibu wa maelezo ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, ACP Théos Badege “ilhali alikuwa amefanya kosa la jinai.”

ACP Badege amesema marehemu alifunguliwa mlango ili aende chooni kujisaidia, akakimbia, na alipokimbia ndipo polisi wakaamua kumfyetulia risasi kwani alikuwa anakabiliwa na kosa kali.

Namahoro alifikishwa kituoni hapo kwa kosa la kumjeruhi afisa usalama wa idara ya DASSO, ambapo inadaiwa alimpiga upanga pajini kumzuia kubomoa nyumba yake iliyojengwa shelabela.

“Polisi walikuwa kazini na hawakuwa na jinsi isipokuwa kumpiga risasi kwani alifanya kosa kubwa, alimjeruhi DASSO kwa kumpiga upanga kwenye paji la uso,” amesema ACP Badege.

“Polisi aliyefyetua risasi alijua uzito wa kosa, halafu na yeye kukimbia alijua amefanya kosa zito,” ameongeza ACP Badege, kulingana na Ukwezi.com

Marehemu Namahoro alikuwa mkazi wa Kata ya Ruganda, Tarafa ya Kamembe huko Rusizi. Anadaiwa kumpa jeraha afisa huyo wa DASSO Jumatano tarehe Aprili 19, 2017.

Majeruhi huyo aitwaye Vénuste Ndahagaze amelazwa hospitalini ambapo anaendelea kushughulikiwa na matabibu.

Vénuste Ndahagaze akiwa kwenye kitanda chake kwa matibabu
Vénuste Ndahagaze akiwa kwenye kitanda chake kwa matibabu
Hiyo ndiyo nyumba ya marehemu Namahoro inayodaiwa kuwa ilikuwa inajengwa shaghalabaghala
Hiyo ndiyo nyumba ya marehemu Namahoro inayodaiwa kuwa ilikuwa inajengwa shaghalabaghala

Angefikishwa mahakamani na kukutwa na kosa la kujeruhi kwa kudhamiria, Namahoro angehukumiwa kifungo cha kuanzia miezi sita hadi miaka miwili jela, na kupigwa faini ya kuanzia faranga laki moja hadi laki tano, kwa mujibu wa kifungu namba 148 cha kanuni za mwenendo wa makosa ya jinai.

Vitendo vya kuwaua wafungwa vimekithiri siku za nyuma nchini Rwanda, ambapo baadhi wameuawa na askari polisi huku wengine wakiuawa na askari magereza katika nyakati tofauti.

Sababu ya kuwapiga risasi zilizosababisha vifo vyao imekuwa ikitajwa kuwa ni wao kujaribu kukimbia kutoka walikofungiwa, au kujaribu kunyang’anya bunduki maaafisa usalama wa taifa.

Weka maoni