Post moja ya Facebook ilivyomfungulia milango ya utajiri mjasiriamali Hassan

477
Mjasiriamali Hassan Habiyambere kutoka Jijini Kigali

Watu wengi hutumia mitandao ya kijamii kupiga soga na ndugu, jamaa na marafiki kuliko kutafuta riziki. Wengine huharibu kazi kwa ‘kuchat’ na imeshakuwa mtindo sehemu nyingi.

Hassan Habiyambere ni mjasiriamali kutoka mjini Kigali ambaye mtaji wa kuwekeza katika biashara ya kuuza na kukodisha magari umeota mizizi katika post aliyorusha Facebook.

Mambo yalivyoanza, rafiki yake alimuomba amtafutie mteja wa gari lake. Mteja alijitokeza baada ya kuona tangazo hilo katika mtandao wa Facebook. Shughuli iliiva, akagharamia.

Hassan alipokea kitita cha faranga elfu 50 kutoka kwa muuzaji huku mnunuzi akimpa faranga elfu laki moja hamsini. “Ilikuwa kama miujiza,” amesema Hassan.

“Katika muda wa lisaa limoja sikutegemea kupata pesa ndefu kama hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa mshahara wangu wa mwezi ulikuwa ni laki moja tu.”

Siku chache baadaye akaja mtu mwingine akitaka amsaidie kama dalali kuuza gari lake. Hapo ikabidi afungue ukurasa wa Facebook wa kufanya matangazo ya magari.

“Mimi sikuwa na gari wala mtaji, ila nikasema lazima niingie mzima mzima katika biashara hiyo ya kuwakutanisha ambao wana magari ya kuuza na wanaotaka kununua,” amesema.

Kijana huyu ambaye ana umri wa miaka 27, alikuwa anafanya kazi huko CBE (Chuo Kikuu cha Rwanda Koleji ya Biashara na Uchumi). Alipopata hiyo pesa ya udalali, akaanza kuweka akiba.

Baada ya miezi michache benki ikampa mkopo wa miliyoni 2,5. Alipojumlisha na akiba aliyokuwa ameweka ndipo akaingia kwenye biashara yenyewe ya uagizaji wa magari.

Kwanza alinunua gari chakavu ambalo alilifanyia matengenezo kabla ya kuliuza. Hapo alipata tijara ya faranga laki tano na baada ya hapo ndipo akajitokeza mteja mwingine kutoka Facebook.

Alitengeneza mkwanja mwingine wa faranga miliyoni tatu baada ya kufaulu kumletea mteja huyo gari alilomuagizia. “Hapo ndipo nikaamua kuacha kazi yangu CBE,” amesema Hassan.

Kilichofuatia ni kuanzisha kampuni yake ya UH CAR DEAL inayojishughulisha na uuzaji na ukodishaji wa magari, kwa mujibu wa The New Times. Ilikuwa mwaka 2014.

Hasaan akiwa ofisini kwake Kigali mjini kati

Pamoja na kwamba alikuwa mfanyabiashara chipukizi ambaye hata hakuwa na mtaji tosha, kijana huyu alijenga uaminifu miongoni mwa wateja akiamini uaminifu ndio ngao.

“Siyo rahisi kuwashawishi wateja mpaka kukuamini wakati hata wewe ni mpya kwenye ramani ya biashara. Ilibidi niwe na tabia nzuri, nisiwazingue wateja ili waniamini,” amesema.

Hassan katika jitihada za kutanua kampuni yake, aliwatafuta washiriki kutoka nchi zingine ambapo leo UH CAR DEAL ndiyo wakala wa SBT, kampuni ya uuzaji magari kutoka Japan.

Na kama haitoshi mwekezaji huyu aliingia mikataba na Al-Futtaim Motors, ambayo ni kampuni inayowakilisha Toyota huko Dubai, huku mikataba mingine ikihusisha makampuni ya Korea.

Ana wafanyakazi 12 wa kudumu, wakiwemo naibu wake na madereva 8, watano wao wakiwa na mishahara ya kila mwezi.

“Lengo langu ni kutoa mchango wangu kuisaidia serikali kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana,” amesema Hassan ambaye ana ndoto ya kuanza kuuza magari mapya katika siku za mbeleni.

Hassan amewashauri vijana kukazana kujiundia ajira kuliko kutegemea kupata kazi kutoka kwa serikali au mashirika ya kibinafsi kwani mtegemea cha ndugu hufa maskini.

“Vijana wanatakiwa wawe na ndoto za kujitengenezea ajira kama wanataka mustakbali mzuri,” amesisitiza Hassan anayeamini kuwa matatizo ni changamoto na changamoto ni muhimu maishani.

Weka maoni