PSG kumtambulisha Neymar kwa ‘mbwembwe’ jumatano

195

Kwa mashabiki wa klabu ya Barcelona huenda wasiamini tetesi za mshambuliaji wao Mbrazil, Neymar Jr kuwa ameitosa klabu yake na kuhamia kwa matajiri wa Ufaransa, Paris Saint-Germain, ukweli ni kwamba dili hilo ni asilimia 98 limeshatiki kinachosubiriwa ni masaa tu atangazwe.

Kwa mujibu wa magazeti makubwa nchini Ufaransa kama L’Équipe na Europe 1 yametangaza kuwa Neymar leo jumanne anaenda Doha, Qatar kuonana na Rais wa klabu hiyo Nasser Al-Khelaifi na kufanyiwa vipimo vya afya.

Zoezi la kumtambulisha na kumtangaza Neymar linatarajiwa kufanyika kesho, jumatano tar 2 Agosti kwa mbwembwe ndani ya jiji la Paris nchini Ufaransa ambapo maelfu ya mashabiki wa klabu hiyo watahudhuria kwenye uwanja wa klabu hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Équipe taarifa zinaeleza kuwa viongozi wa klabu hiyo wapo kwenye mazungumzo na Meya wa jiji hilo kuomba kibali cha kuweka picha kubwa ya Neymar kwenye mnara maarufu zaidi duniani ulio katikati ya jiji hilo ujulikanao kwa jina la  Eiffel kama walivyowahi kufanya kwa Zlatan Ibrahimovic walivyomsajili akitokea Barcelona.

Uhamisho wa Neymar kutoka Barcelona umeripotiwa kuwa ni wa Euro Milioni 193 na kama itatokea utakuwa ndio usajili wa ghali zaidi duniani kuwahi kutokea katika historia ya mpira wa miguu.

Hata hivyo taarifa hizo za Neymar kuhama Barcelona zinashika kasi kwa kile kinachoonekana kuwa klabu hiyo imeshindwa kumlipa baba yake mzazi na Neymar, Neymar Sernior ambaye ndiye meneja wake kiasi cha Euro Milioni 26 kama masharti ya mkataba yalivyoeleza.

Katika mkataba alioingia na Barcelona akitokea Klabu ya Santos ya Brazil, unaeleza kuwa kama Neymar akiongeza mkataba mpya na Barcelona, basi baba yake huyo ambaye ni meneja wake anapaswa kulipa kitita cha euro milioni 26.

Weka maoni