‘Queen of Social Media’ Wema Sepetu atua Rwanda kwa ajili ya KFM IG Party

455
Wema Sepetu akiyajibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kilichomleta Rwanda

Miss Tanzania 2006 ambaye anajitambulisha pia kama ‘Queen of Social Media’ (Malkia wa Mitandao ya Kijamii), Wema Abraham Sepetu, ametinga Rwanda jioni ya leo, Jumatano.

Muigizaji huyo wa filamu za kibongo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kwenye ulingo wa filamu, amekuja Rwanda kwa ajili ya KFM Instagram Party, tamasha litakalowakutanisha watumiaji wa mtandao wa Instagram Novemba 24, 2017, Chillax Lounge, Nyarutarama.

Wema Sepetu wakati anafika Chillax Lounge kukutana na waandishi wa habari kwa mahojiano

Wema Sepetu (@wemasepetu) ambaye ana wafuasi (followers) zaidi ya miliyoni tatu na laki mbili Instagram, amewataka watumiaji wa mtandao huo wa kijamii kuutumia vizuri na siyo kudhalilishana au kusababisha matatizo kwenye jamii ambayo pengine wangeweza kuyaepuka.

Wema akiyajibu maswali ya waandishi wa habari mjini Kigali

Muda mfupi baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kigali, Wema amekutana na waandishi wa habari ambapo wamemuuliza maswali kibao yahusuyo hasa kazi zake kama msanii na jinsi anavyotumia mitandao ya kijamii pia kuwasiliana na mashabiki wake na pia kutangaza kazi zake.

Ndiyo mara ya kwanza Rwanda amefika nchini Rwanda. Amesema amependa ilivyo safi.

Wema Sepetu au Sepenga kama watu wanavyopenda kumuita kwa utani, amesema amefurahi kuanza kujionea vitu ambavyo amekuwa akiambiwa kuhusu Rwanda kuwa ni nchi ambayo ni ndogo kieneo lakini yenye usafi usioelezeka.

“Ndio mara yangu ya kwanza nimekuja (Rwanda) ndege imegusa ardhi saa mbili na nusu naweza kusema sina hata lisaa tangia nimefika, vile nimekuwa nikisikia kuhusu Rwanda nimeviona, najua bado ni usiku kesho nitaweza kuona mengi zaidi, nimesikia kwamba Rwanda ni nchi ambayo ni ndogo lakini ni nzuri, nilikuwa niko na kaka yangu tunapisha barabarani napigwa na butwaa ‘oh my God hii sehemu ina usafi mwingi’,” amesema Wema.

Waandishi wa habari walikuwa wamejitokeza kwa wingi kuzungumza na mrembo huyo kutoka Tanzania

Alipoulizwa nini watu watarajie kukipata kutoka kwake katika tamasha lililomleta, amewataka wake wakae mkao wa kula kwani wataruhusiwa kukaa naye wapige soga na waweze kushauriana mambo mengi hususan yale yahusuyo matumizi stahiki ya mitandao ya kijamii.

Amesema, “Ni jambo jema kwamba nimekuwa Queen of Social Media, siyo kwamba nimejipa mwenyewe, watu wamenipa hicho cheo, naamini itakuwa ni muda mwafaka wa watu kukutana nami ana kwa ana, kwa sababu kuonana kwenye ‘ma-social media’ tu mtu anakuwa anatamani kukuona, eti huyu Wema natamani nikae naye nipige naye picha, tupige naye stori mbili tatu, sitaweza kufanya hivyo na watu wote ila angalau watu waweze kupata taswira halisi kuhusu mimi kipenzi cha wengi kutoka Tanzania.”

Mrembo huyu amesema watu wanaomkubali watakuwa na muda wa kutosha wa kumupiga naye stori na kupiga picha naye pia

“Mimi ni mcheshi, napenda burudani napenda matamasha naamini nitafurahi kuwa na watu wangu wa Rwanda hasa ukizingatia huu mwaka unaelekea ukingoni, 2017 ni mwaka ambao kwangu mimi umekuwa ni mrefu sana, pia nashukuru Mungu unaisha,” ameongeza.

Wema Sepetu alianza kuigiza tangu akiwa shule ya msingi, lakini alikuja kuingizwa rasmi kwenye tasnia ya filamu na aliyekuwa mpenzi wake Steven Kanumba kipindi wakiwa na uhusiano.

Filamu ya Point of no Return aliyoigiza akiwa na Kanumba ndiyo iliyomfumbua macho na kumfanya atambue kipaji chake kilivyo kikubwa, na baada ya hapo ndipo akashiriki filamu mbalimbali zilizofanya vizuri ikiwemo Family Tears, Red Valentine na nyinginezo nyingi ambazo zilimvutia sifa ya muigizaji mzuri wa kike Tanzania.

Weka maoni