Rais Kagame aahidi kuachia madaraka mwaka 2024

685
Rais Kagame amesema ataondoka madarakani mwaka 2024

Uchaguzi mkuu nchini Rwanda utafanyika Agosti 3, 2017, kwa Wanyarwanda walio nje ya nchi yao, na kesho yake ndipo Wanyarwanda walio nchini humu watadamkia kupiga kura kuchagua rais wao.

Bila shaka Rais Kagame atashinda uchaguzi na ni ushindi ambao umekuwa ukitabiriwa kwa muda mrefu.

Mwaka 2015 Wanyarwanda wapatao miliyoni 4 ambao ni zaidi ya asilimia 70% ya wapiga kura, walipaza sauti zao kulitaka bunge lirekebishe katiba ili Kagame apate haki ya kuwania urais kwa mara ya tatu.

Bunge lilifanya hivyo, na halikuishia hapo kwani lilimruhusu rais huyo ambaye ana umri wa miaka 59 kuwania awamu zingine hadi mwaka 2034. Ikumbukwe kwamba aliingia madarakani mwaka 2000.

Rais Kagame amelihakikishia gazeti la Jeune Afrique kuwa awamu hii ya miaka saba ndiyo ya mwisho na Wanyarwanda wanatakiwa waanze kufikiri kuhusu atakayewaongoza baada ya 2024.

Alipoulizwa kama ataachia madaraka itakapofika ukingoni awamu hii ya miaka 7, Rais Kagame amesema lazima atafanya hivyo, na ni suala ambalo ataeleza kinagaubaga wakati wa kampeni za uchaguzi.

“Inawezekana natakiwa niliangazie suala hili katika siku chache zijazo nitakapoanza mbio za urais. Kuna aina ya makubaliano kati yangu mimi na RPF-Inkotanyi kwa upande mmoja, na raia wa Rwanda kwa upande mwingine.”

“Raia, kupitia kura ya maoni ya Disemba 2015, waliniomba niendelee kuwaongoza nikakubali, ila muda mwafaka wa kuwaambia waanze kufikiri nje ya uwezo wangu umewadia”  ameongeza Rais Kagame.

Kiongozi wa chama pekee cha upinzani cha Democratic Green Party of Rwanda (DGPR), Frank Habineza (wa pili kushoto) akiwa katika Mahakama ya Rufaa akiiomba ikataze bunge kurekebisha katiba, ombi lililogonga mwamba (Picha/Igihe)

Ukifumbia macho historia ya Rwanda na kuchambua maendeleo yake kwa vigezo vya mataifa ambayo hayakuwa na historia mbaya kama Rwanda, kamwe hutaelewa chochote, amesema Rais Kagame.

Kipindi cha kampeni za uchaguzi ni kipindi ambacho wagombea hutoa ahadi za yale watakayoyafanya ili wapate kura za wananchi. Kagame hana jipya la kuwaahidi wananchi isipokuwa tu kuwataka waungane.

“Siwezi kutoa ahadi hewa na sina la kuwaahidi Wanyarwanda ukiacha kuwataka washirikiane bega kwa bega kwa ajili ya mustakbali mzuri,” amesema Rais Kagame akihojiana na Jeune Afrique.

Alipoulizwa kama anajua ukweli kwamba yeye ndiyo nguzo ya msingi katika mfumo wa uongozi wa Rwanda na bila yeye taifa linazama kama meli ambayo haina nahodha, Rais Kagame alimuambiwa mwandishi wa habari kwamba Wanyarwanda hawako hivyo, kwamba Wanyarwanda ni jamii inayoweza kuendelea kuwepo na kustawi akiwepo au asipokuwepo.

Bi Uwiragiye Emerence alisema atajitia kitanzi iwapo Kagame hataendelea kuiongoza Rwanda.

“Ingawaje raia wa Rwanda walitaka niendelee kuwaongoza, lakini ustawi wao utaendelea kuwepo hata baada ya mimi kutoweka,” ameongeza.

Kagame aliongoza majeshi ya RPA yaliyoiangusha serikali ya MRND iliyoratibu na kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi. Ni mauaji yaliyogharimu maisha ya watu zaidi ya miliyoni moja katika kipindi cha miezi mitatu tu, Aprili-Julai 1994.

Hakupita anakalia kiti cha urais kwani alipewa kiti hicho Pasteur Bizimungu, ambapo Kagame alikabidhiwa wadhifa wa Waziri wa Jeshi na Makamu wa Rais katika serikali ya mseto.

Baada ya miaka sita, Pasteur Bizimungu alilazimika kujiuzulu. Kagame ambaye alikuwa anachukuliwa na Wanyarwanda kama mkombozi aliyetamatisha mauaji ya kimbari, ndiye alichukua nafasi ya Bizimungu.

Pasteur Bizimungu akiongea na mwandishi wa habari kuhusu nyumba yake iliyoko Kacyiru mjini Kigali ambayo ilishika moto sehemu ndogo mwaka 2016. Baada ya kujiuzulu mnamo mwaka 2000 alikabiliwa na tuhuma za kuunda kundi la kigaidi na kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 ambapo alikuja kuachiwa huru kwa msamaha wa rais Kagame.

Katika uchaguzi wa kwanza alioshiriki kama mgombea miaka mitatu baada ya kuingia madarakani, Rais Kagame alipata asilimia 95 ya kura kabla ya kupata asilimia nyingine 93% miaka saba baadaye.

Amekuwa akituhumiwa na mashirika ya kupigania haki za binadamu kwa kutumia mabavu na kuminya uhuru wa vyombo vya habari, huku mashirika mengine yakimsifia kwa kuliinua taifa lake kiuchumi.

Safari hii anatarajiwa kushindana na Frank Habineza kutoka chama cha DGPR huku wagombea wengine kisimama kama wagombea binafsi, na hao ni pamoja na Philippe Mpayimana na Diane Rwigara.

Kiongozi wa Chama cha Democratic Green Party of Rwanda, Frank Habineza

Nchini Rwanda kuna chama kimoja tu cha upinzani ambacho ni Democratic Green Party of Rwanda (DGPR). Vyama vingine vya upinzani havijapata kusajiliwa rasmi.

Rais Kagame amesema “Rwanda ni nchi ya haki. Jukumu langu siyo kuunda vyama vya upinzani, bali kujenga mazingira mazuri ya uhuru wa maoni. Mambo mengine yanafuata utaratibu wa sheria.”

Mwaka 2015 wakati wa kuelekea kurekebishwa kwa katiba, raia wengi walisikika wakionyesha wasiwasi wa usalama wao kuingia mashakani iwapo Rais Kagame hataendelea kuliongoza taifa hili.

Ilisikika sauti moja ya mwanasiasa mmoja tu akisema ana uwezo wa kuiongoza Rwanda, ambaye ni Bw Habineza wa Green Party.

Philippe Mpayimana na Diane Rwigara ambao wameshatangaza nia ya kugomea urais mwaka huu, ni watu ambao majina yao ndipo yanaanza kuchipuka kwenye shamba la siasa nchini Rwanda.

Bw Mpayimana aliwahi kuwa mwandishi wa habari akiwa ukimbizini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alikoishi kabla ya kuelekea Paris, Ufaransa.

Philippe Mpayimana aliishi Ufaransa mpaka alipoamua kurudi nchini Rwanda kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaokaribia

Diane Rwigara, ni mtoto wa kike wa tajiri Asinapol Rwigara aliyefariki katika ajali yenye utata ya barabarani mapema Februari ,2015. Alianza kupata kujulikana nchini baada ya kifo cha baba yake.

Alisikika mara kibao akiinyoshea kidole serikali kuwa ndiyo iliratibu mauaji ya baba yake baada ya yeye kufarakana nayo, madai ambayo serikali iliyatupilia mbali ikiyataja kuwa hayana ukweli wowote.

Diane Rwigara ameanza kuikosoa serikali baada ya baba yake kufariki dunia katika mazingira ya kutatanisha

Siku mbili tu baada ya kutangaza nia yake ya kugombea urais, picha zake za utupu zilivuja mitandaoni.

Ingawaje uchaguzi haujafanyika, wachambuzi wanaamini Rais Kagame ndiye atakayepata kura nyingi na hivyo kuweza kuliongoza taifa hili la Afrika ya Kati kwa mhula mwingine wa miaka 7.

Ni taifa ambalo Rais Kagame anasifika kwa kuliendeleza kiuchumi na kimiundombinu.

Leo hii asilimia  91% ya wanyarwanda wana bima ya afya.

Kigali inaaminika kuwa miongoni mwa miji safi zaidi barani Afrika.

Kigali ni miongoni mwa majiji yanayotajw akuwa na usafi zaidi barani Afrika

Rwanda ni nchi ya nne kwa kuwa na kiwango cha chini cha rushwa barani Afrika, kwa mujibu wa ripoti ya Transparency International.

Weka maoni