Rais Kagame awaasa Wanyarwanda kujenga umoja na kujitegemea

368

Rais wa Rwanda Paul Kagame jana aliwahutubia Wanyarwanda waishio barani Ulaya waliokuwa wamekusanyika mjini Brussels, kuhusu wanachotakiwa wafanye ili Rwanda ipate maendeleo endelevu.

Rais Kagame aliitaja Rwanda kuwa ni nchi ambayo misingi ya maendeleo yake ni umoja na mshikamano baina ya wananchi, hasa baada ya kupitia historia ngumu ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyogharimu maisha ya watu zaidi ya miliyoni moja mwaka 1994.

“Tunajenga mustakbali mzuri kwa ajili ya taifa letu, ule ambao misingi yake ni umoja, kujituma, ukweli na kujitegemea,” alisema.

Rais Paul Kagame akiongea na Wanyarwanda huko Ubeljiji mjini Brussels

Rais wa Rwanda amewataka Wanyarwanda watafakari kuhusu kwa nini nchi yao iendelee kuwategemea wahisani ambao mara nyingi walisikika wakisema wanaweka mbele maslahi yao.

“Tunatakiwa tujiulize hata kwa nini wanatakiwa watujali. Inatukumbusha jukumu letu la kuishi maisha ya kujitegemea. Hatutakiwi kusubiri tujaliwe na watu wengine”

“Historia yetu ilitufudisha hasa pale ambapo ilibidi tujikomboe, ilitupa fundisho kwamba tunatakiwa kujitegemea sisi wenyewe,” aliongeza rais Paul Kagame.

Aisha rais Kagame amesema Waafrika waishio barani Ulaya wana jukumu la kushiriki katika maendeleo ya nchi yao kwani wamepata elimu ambayo mataifa yao yanahitaji ili yaendelee.

“Kuishi nje ya nchi yako haimaanishi kusahau nyumbani kwako. Unaweza kutumia unachopata kujenga nchi yako ukiwa huko uliko,” alisema.

Waziri wa nchi za nje Bi Louise Mushikiwabo ambaye pia ni Msemaji wa Serikali ya Rwanda, amesema Rwanda ni nchi ya furaha kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo iliongozwa kwa sera za chuki na ubaguzi.

“Rwanda ni nchi iliyotaabika kutokana na historia ya ubaguzi, ila leo ni nchi ambayo inapiga vita ubaguzi na utengano,” ameuambia umati wa watu waliojitokeza kwa ajili ya Rwanda Day.

Kila mwaka Rais Kagame huwatembelea Wanyarwanda waishio nje ya nchi yao hasa Barani Ulaya na Amerika, na siku hiyo ndiyo huitwa Rwanda Day kwa Kiingereza.

Rais Kagame akiongea na raia huku Balozi wa Rwanda nchini Ubeljiji Olivier Nduhungirehe akitabasamu

Katika hatua nyingine Bi Louise Mushikiwabo amewahamasisha Wanyarwanda kuchangamkia fursa za kimaendeleo zinazopatikana nje ya nchi yao, na pia kuwakaribisha wawekezaji nchini mwao.

“Kila Mwafrika anakaribishwa kwa ukarimu nchini Rwanda. Rwanda inaamini katika muunganiko wa Waafrika na ndiyo maana tukawafungulia milango Waafrika,” ameongeza.

Wanyarwanda waliohutubiwa walipewa muda wa kutoa maoni na kuuliza maswali, ambapo baadhi walichukua fursa hiyo kumshukuru Rais Kagame wakisema uongozi wake ni mzuri.

Kwa picha zaidi bonyeza hapa

Weka maoni